Safina Sarwatt,Moshi
Madiwani wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Diwani wa Kata ya Uru Shimbwe, Bertin Mkami na Diwani wa Viti Maalumu, Kata ya Uru Mashariki, Elizabeth Temba katika Halmashauri ya Wilaya Moshi Vjiijini wamejiuzulu nafasi zao na kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichokidai kuchoshwa na migogoro ndani ya chama.
Wakizungumza wakati wakipokelewa leo Mei 2, na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi na kuwakabidhi kadi za CCM madiwani hao wameeleza sababu za kuhama chama hicho ni kuchoshwa na migogoro ndani ya chama na mienendo ya viongozi wa chama hicho.
Kwa upande wake Mkami amesema sababu za yeye
kujivua nafasi yake ya udiwani ni kutokana na mwenyekiti wa baraza la madiwani halmasahuri kuitenga kata yake katika suala la maendeleo.
“Kata ya Uru Shimbwe imetengwa kabisa katika suala la kimaendeleo Mwenyekiti na Mbunge hawasikilizi kero za wananchi wa kata yangu nimeona ni vyema nikajiuzulu kwani sioni sababu za kuendelea kuwa diwani wakati wananchi wanateseka, ndiyo maana nimeamua mwenyewe kujiunga na CCM ili nikawatumikie wananchi,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Kastori Msigala amekiri kupokea barua za madiwani hao ya kujiuzulu nafasi zao na ataziwasilisha barua hizo TAMISEMI ambako watazipeleka Tume ya Uchaguzi (NEC) na nafasi hizo zipo wazi kwa sasa .
Aidha Mwenyekiti wa CCM Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema chama hicho kimeendelea kuwapokea wanachama wapya kutoka Chadema nahili linatokana na utendaji kazi wa serikali iliyopo madarani.
“Serikali ya CCM imeonyesha imani kubwa kwa wananchi kutokana na kutekeleza miradi kubwa ndani ya muda mchache,” amesema Boisafi.