22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Meatu wavutana ongezeko gharama za matibabu

Na Derick Milton, Meatu

Madiwani wa Halmashuari ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, wamepitisha uamuzi wa kuongeza gharama za matibabu kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya kwenye halmashauri hiyo, ambapo kuanzia sasa mgonjwa mwenye uhitaji wa huduma ya upasuaji mdogo atalazimika kulipa Sh 30,000.

Mbali na huduma hiyo, mgonjwa kumuona daktari kwa ajili ya matibabu atalazimika kulipa Sh 3,000 ikiwa ni ongezeko la Sh 1,000 kutoka Sh 2,000 ya awali.

Madiwani hao wamefikia uamuzi huo Ijumaa Oktoba 29, 2021 kwenye kikao cha Baraza la halmashuari hiyo, ambapo wamesema sababuya ongezeko hilo ni kutaka kupambana na changamoto ya ukosefu wa dawa ambayo inavikabili vituo vya kutolea huduma za Afya kwenye Halmashauri hiyo.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, ambao uliamuliwa kwa madiwani hao kupiga kura za ndiyo na hapana, baadhi walionekana kupinga ongezeko hilo kwa kile walichoeleza kuwa linakwenda kuwa mwiba kwa wananchi wenye hali duni.

Baadhi yao licha ya kukubali pendekezo hilo, walitaka lisianze kutekelezwa kwa sasa, hadi timu ya watalaamu wa Afya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashuari hiyo watoe elimu kwanza kwa wananchi ambao ndio watumiaji wa huduma hizo.

Miongoni mwa madiwani waliopinga ongezeko hilo ni Consolatha Lushu (CCM) ambaye amesema kuwa utekelezwaji wake utakuwa changamoto kwa wananchi na kwamba linakwenda kuwaumiza ikiwamo kutishia chama chake kupata kura katika uchaguzi ujao wa 2025.

“Mmesema kuwa hoja hapa ni kuongeza mapato ya vituo, kwani CHF imeshindwa kusaidia?” amehoji Consolatha na kuongeza kuwa:

“Kabla ya kufikia uamuzi huu wa kuongeza gharama mlijiuliza kwa nini CHF imegoma, naomba jambo hili tulisitishe kwanza na linaweza kutuletea tatizo sisi wenyewe,” amesema.

Kwa upande wake diwani, Njile Ngwakwa, aliwataka madiwani hao kukubali ongezeko hilo lakini utekelezaji wake usitishwe kwanza mpaka pale wananchi watakapopewa elimu ya lengo la kuongeza gharama hizo.

Diwani Paul Matembele wa kata ya Mwamanimba, amewataka madiwani hao kukubali pendekezo hilo, kwani linakwenda kkuleta mwarobaini kwa wananchi wa halmashuari hiyo ambao wamekuwa wakilalamika mara kwa mara juu ya kukosa dawa.

“Tumekuwa na changamoto kubwa ya vituo vyetu kukosa dawa mara kwa mara, na wananchi wamekuwa wakilalamika sana, njia hii itakuwa mwarobaini wa tatizo hili kwani inakwenda kuongeza mapato ya vituo vyetu,” alisema Matendelea.

Mwenyekiti wa halmashuari hiyo, Anthony Philipo akihitimisha mjadala huo, amesema ongezeko hilo halitawahusu wajawazito ambao watakuwa na uhitaji wa kufanyiwa huduma za upasuaji kwa ajili ya kujifungua, kutokana na sera kueleza huduma kwao ni bure.

Licha ya maelezo hao mabishano yaliendelea hali ambayo ilimpelekea Mwenyekiti huyo kuamua kupigwa kura za siri, ambapo waliosema ndiyo ni madiwani 27 huku 12 huku 12 wakisema hapana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles