Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka madereva wa malori nchini kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni mbalimbali zinazosafirisha mizigo nje ya nchi waliofika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Mabibo, Dar es Salaam kupima kama wana maambukizi ya virusi vya corona au laa.
Waziri Ummy alisema ugonjwa wa corona bado upo ingawa maambukizi yamepungua na kwamba jambo la muhimu ni wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.
“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima virusi vya corona, kama mtakutwa hamna maambukizi ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi, malimao, mboga za majani na tangawizi, hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,’’ alisema Ummy.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Ambele Mwafulango alisema pamoja na kupima vipimo vya wagonjwa wengine, kwa upande wa madereva walioko Dar es Salaam kwa siku wanawapima 200 na kwa madereva walioko mikoani kuna utaratibu maalumu wa kuchukuliwa sampuli ambazo zinatumwa Dar es Salaam kwa vipimo.
“Majibu ya vipimo yanatoka baada ya masaa 48, kama madereva hao watakutwa hawana maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14, hii itawasaidia kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi bila ya kupimwa tena katika nchi wanazokwenda,” alisema Mwafulango.
Alisema kabla madereva hao hawajafanyiwa vipimo vya corona wanapimwa joto la mwili na wale ambao watakutwa na joto la juu la mwili, watapewa huduma ya haraka zaidi ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.
“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizi ya ugonjwa wa corona, tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote.
“Katika maabara hii ya Mabibo tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya masaa 24 zinapima vipimo 1,800. Hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es Salaam ambapo tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,’’ alisema Mwafulango.