30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Nyota Yanga kuwekwa kitimoto

Na WINFRIDA MTOI, Dar es Salaam

UONGOZI wa Klabu ya Yanga na wadhamini wao GSM, wanatarajia kukutana na wachezaji leo kupanga mikakati ya maandalizi ya kurejea dimbani katika mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tangu marufuku ya michezo iliyowekwa na serikali ya kuzuia shunguli zote za michezo, timu hiyo haijakutana zaidi ya kila mchezaji kufanya mazoezi binafsi.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro, alisema lengo kubwa la kukutana pande zote tatu ni kukumbushana majukumu ya kila mmoja katika kuhakikisha wanafanya vizuri Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam.

“Lazima tuwe na ushiriki mzuri katika mashindano yote, hivyo tumeona tuitishe kikao maalum cha pamoja kuhakikisha  kunakumbushana wajibu na kunapeana mikakati ya namna ambayo tutafanikisha mipango yetu,” alisema Kandoro.

Alisema baada ya kikao hicho, benchi la ufundi litaendelea na taratibu zake likianza kuwapima wachezaji afya na uzito kabla ya kuanza mazoezi rasmi.

Alieleza kuwa maandalizi ya uwanja wa mazoezi yameshafanyika, wataendelea kufanyika Chuo Cha Sheria kama ilivyokuwa awali na endapo vipimo vitakamilika Jumatano wanaanza rasmi kujifua.

Alisema lengo lao ni kufanya mambo mazuri, yatakayomfurahisha kila Mwanayanga ikiwamo kuchukua ubingwa wa kombe shirikisho.

Kandoro alisema anaamini wachezaji wamezingatia kile walichokuwa wanaelekezwa na mwali, wakati akitoa program za mazoezi ya binafsi na viongozi wa benchi la ufundi waliokuwepo walikuwa wanawafuatilia.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Frederick Mwakalebela, aliwataka Wanayanga kutulia katika kipindi hiki, kwani ni muda wa Yanga kufanya mambo makubwa.

Mwakalebelea alisema miongoni mwa mambo hayo, ukiacha usajili ni mchakato wa mabadiliko ambao upo katika hatua nzuri, hivyo wasiyumbishwe na watu.

“Tunafahamu kuna watu wanapinga, lakini sisi tunaangalia maslahi ya klabu na makubaliano ya wengi, tunawaomba Wanachama na wadau wa Yanga waunge mkono kile kinachofanywa na uongozi, wasikubali kurudishwa nyuma,” alisema.

Alisema kamati ndogo inayoongozwa na Alex Mgongolwa, imefanya kazi kubwa na inaendelea na kazi ya kuhakikisha unapatikana mfumo sahihi wa uendeshaji wa klabu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles