27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Zungu ataka teknolojia kutibu tope sumu migodini

Na MWANDISHI WETU-MARA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu, amewataka wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kutumia teknolojia rafiki ya CIP gold processing, kulinda mazingira nchini kama njia ya kupunguza gharama za utunzaji wa mazingira kwa mgodi husika.

Waziri Zungu ameyasema hayo jana baada ya kukagua bwawa la mgodi linalohifadhi tope sumu, akiambatana na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Profesa Esnati Chaggu na watendaji wa baraza hilo.

“Ni muhimu teknolojia hii itumike kutibu tope sumu katika migodi yote kwani athari zake ni kubwa endapo sumu hii itaingia katika mito na kuhatarisha afya za wananchi,” alisema Zungu.

Alisema ni kweli Serikali inathamini uwekezaji ili kukuza uchumi, lakini uwekezaji lazima uzingatie sheria na kanuni za kutunza na kuhifadhi mazingira ya Tanzania ili yapatikane  maendeleo endelevu.

“Tumejiridhisha usalama wa maji taka upo na mara kwa mara tunahakikisha  tunafanya ukaguzi ili maji taka haya yasiwaathiri wananchi waliouzunguka mgodi huu,” alisema Zungu.

Alisema kwamba migodi ina kila sababu ya kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira katika kutibu maji taka yake kwani kufanya hivyo kutalinda afya za wananchi wanaoizunguka na kuondoa migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

“Nimeambatana na Naibu Waziri wa Ardhi na Waziri wa Madini kwa lengo la kusikiliza changamoto za wananchi na wawekezaji,  ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi maeneo haya,”  alisema Zungu. 

Kwa upande wake Waziri Biteko amekabidhi hundi ya Sh bilioni 34 ikiwa ni malipo ya fidia kwa wananchi wa eneo la Nyamongo ili kuondoa migogoro kati yao na Kampuni ya Barrick. 

“Baada ya malipo haya, tunaamini hakutakuwapo  mgogoro tena. Kadhalika Serikali  haitavumilia watu watakaochochea migogoro kati ya wananchi na mgodi huu,” alisema Biteko.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mabula, aliwataka wananchi kufuata taratibu za mipango miji kupitia halmashauri zao ili kuepukana na ujenzi holela ambao unakwamisha juhudi za kuhifadhi na kutunza mazingira.

“Nawaomba wananchi waache tabia ya kujenga nyumba za kutegesha ili baadaye walipwe fidia. Ikumbukwe  kwamba kwa upande mwingine  kufanya hivyo kunaweza kuwakosesha haki zao za msingi kutokana na kutofuata taratibu za mipango miji,” alisema Mabula.

Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka aliwahakikishia Watanzania kwamba wanayafanyia kazi malalamiko ya wananchi wanaozunguka migodi na kwamba wanaikagua yote nchini kuona iwapo taratibu za kulinda mazingira zinafuatwa.

“Barrick North Mara ni miongoni mwa migodi tunayofuatilia kuhakikisha uendeshaji wake hauleti madhara kwenye mazingira na wananchi wa maeneo ya jirani,” alisema Dk. Gwamaka.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,608FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles