26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Madeni ya Bodi ya Mikopo mzigo kwa wahitimu

Naomi Mwakilembe

Kila mzazi hutamani kuona mtoto wake anafaulu na kuendelea mbele kimasomo. Kama mtoto huyo atafika chuo kikuu mzazi huyo hutamani kuona anapunguziwa mzigo wa ada kwa kupata mikopo ya serikali kupitia Bodi ya Mikopo. Mwanafunzi hutakiwa kuanza kuilipa mara apatapo kazi.

Kwa ujumla Mikopo hii ya elimu ya juu imekuwa msaada mkubwa,kwa kuwapunguzia wazazi wengi mzigo wa kusomesha watoto.

Mzazi anapoona mtoto kapata mkopo hushukuru kwani kutokana na hali ngumu ya uchumi si rahisi kwa wazazi wengi kulipia ada za mamilioni ya shilingi ili kumwezesha mtoto kuendelea na masomo.

Lakini urejeshaji wa mikopo hiyo umekuwa mgmu kwa wahitimu wengi. Kwanza kutokana na ukweli kuwa ajira zimekuwa za shida kupatikana,  wahitimu wengi wamekuwa hawana  vipato. Hii imewafanya wengi wao washindwe kurejesha mikopo hii kwa wakati. Pili, mfumo wa elimu yetu haujaweza kuwaandaa wahitimu wengi kuweza kujiajiri hivyo wahitimu wengi hawana uwezo wa kujiajiri.. Hivyo wahitimu wengi wanakosa mawazo mazuri juu ya nini wanaweza kufanya ili kujipatia vipato. Lakini pia kukosa mitaji ya kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kujiajiri pia ni changamoto.

Hali hii imesababisha urejeshaji wa mikopo hii kuwa ya mashaka kwa wahitimu wengi bado wanasubiri ajira ili waweze kuirejesha. Lakini pia wanaobahatika kupata ajira,  vipato vyao ni vidogo mno; hivyo kusababisha  kuongezeka kwa madeni yao.

Aidha,  wahitimu hawa pia wana mizigo ya kusaidia familia zao; hasa wazazi ambao wanawategemea. Hivyo, urejashaji wa mikopo hii hasa kutoka  kwa wale ambao wana vipato vidogo utaendelea kuwa ndoto.

Hali imezidi kuwa ngumu baada ya Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo imeweka msisitizo katika ukusanyaji mapato,  kuamua kupandisha makato  mkopo kutoka asilimia 8 hadi asilimia 15  kwa mwezi. Uammuzi huo nao  umemeleta changamoto kubwa  ingawa hii siyo shabaha kuu ya  makala hii.

Changamoto kubwa ya mikopo hii  inahusu  riba wanazopaswa  kulipa ikiwa ni pamoja na tozo ya kuchelewa kulilipa.

Mhitimu mmoja akiongea kwa majonzi alisema ‘Nimeanza kulipa marejesho bodi ya mikopo kutoka mwaka 2014 lakini cha kushangaza ni kuwa deni langu linaendelea kukua kila  mwaka.’’

Aliendelea kusema kuwa alipoenda Bodi ya Mikopo  alielezwa kuwa hii  inatokana na utaratibu wa kuthaminisha fedha ya mkopo iliyotolewa kipindi alipokuwa anasoma kwa thamani ya ukopeshaji ya sasa, kwa kiingereza ‘value of retention fee’.

Matokeo yake ni kuwa  licha ya kwamba alianza kuulipa miaka mitano iliyopita lakini deni lake linazidi kukua? Hivyo wakati anakumbuka kuwa alipokea mkopo wa shilingi milioni saba ( alipoanza kusoma mwaka 2011! Ilipofika mwaka 2014 deni lake likikuwa limepanda kufikia  shilingi  milioni 10. Huku akiendelea kulipa deni lake, ilipofika mwaka 2018 aligundua kuwa lilikuwalimeongezeka hadi kufikia shilingi milioni 11.

Ikumbukwe kuwa mdaiwa huyu  anapaswa pia  kulipia kodi ya pango, bili za maji, umeme, taka pamoja na gharama za usafiri wa kila siku kwenda na kurudi kazini  kwake. Pia anatakiwa kuilisha, kuivalisha, kuisomesha familia yake n.k.

Kwa hali hii mtu unajiuliza je, ni lini mtu huyu atamaliza kulipa mkopo wake? Ni lini ataondokana na deni hili ambalo linaendelea kumkandamiza kiuchumi? Hiyo asilimia 15 inayokatwa kwenye mshahara wake mdogo, itamwezesha lini na vipi kuutua huu mzigo huu wa deni linalokua kila mwaka?

Je, mikopo hii ililenga kutoa msaada au ni chanzo tu cha mapato kwa Serikali? Ukataji wa riba na faini hauwasaidii wakopaji  hususani wanaotoka katika familia maskini, kwani huwakandamiza kwenye dimbwi la umasikini.

Je, ni kweli serikali  imemsaidia au imemuongezea shida katika maisha yake? Maana upo uwezekano mkubwa wa mdaiwa kushindwa kabisa kumaliza deni lake kwani kila mwaka linaongezeka. Katika mazingira haya kuna uwezekano mkubwa baadhi ya wadaiwa watakufa huku wakiendelea kudaiwa na Bodi ya Mikopo.

Serikali ingerekebisha vifungu vya sheria vinavyoipa  mamlaka  Bodi ya Mikopo kutoza  riba  ya asilimia 15 pamoja na faini kwa wadaiwa ambao walichelewa kuanza kulipa mikopo yao kutokana na ukweli kuwa  walikuwa hawajapata kazi!

Aidha, wazazi na walezi wenye uwezo wa  kuwalipia watoto wao gharama za masomo ya elimu ya juu bila kuitegemea Bodi ya Mikopo, ni vema wakafanya hivyo ili kuwapunguzia watoto wao dhahama ya kuja kudaiwamadeni makubwa hapo baadae wakati  wakitakiwa pia kuendeleza familia zao.

Mikopo hii  inawaacha wakopaji wengi katika hali mbaya na tegemezi. Wengi wanaendeleakuwa ombaomba wa  misaada kutoka kwa wazazi au walezi wao au hulazimika kuendelea kukopa bila malengo. Ni dhahiri kuwa vijana hawa hawataweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu kwani wanaishi maisha ya kubaingaiza kutokana na mzigo wa madeni yasiyolipika kirahisi ya Bodi ya Mikopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles