NA DAMIAN MASYENENE
– SHINYANGA
SERIKALI imesema imefikia makubaliano na wanunuzi wa pamba kuwa ifikapo Desemba 8, walipe Sh bilioni 47 ambazo ni madeni ya wakulima wa pamba.
Makubaliano hayo yalifikiwa juzi katika kikao kilichokaa kwa saa sita kati ya Serikali na wadau wa zao la pamba kilichofanyika mkoani Shinyanga kikihudhuriwa na wakuu wa mikoa inayolima zao hilo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema changamoto zilizojitokeza msimu uliopita hazitakuwapo msimu ujao.
Alisema kila mkulima atalipwa fedha zake moja kwa moja katika akaunti yake ya benki na kupata pembejeo kwa mkopo, huku akitoa onyo kwa viongozi wa Amcos kutowalazimisha wakulima kulipia mbegu.
“Wilaya zote ambazo wakulima wake hawajalipwa pesa, wahakikishe Amcos zote zina akaunti benki, na hili ni agizo tumelitoa na zoezi hili lifanywe Jumamosi (jana).
“Fedha hizo za wanunuzi zipelekwe kule alafu wakuu wa wilaya wasimamie kulipwa kwa wakulima, kampuni zote zinazodaiwa baada ya kulipa basi wapeleke taarifa hizo kwa wakuu wa wilaya.
“Gari zote za mbegu zikifika wilayani ziripoti kwa wakuu wa wilaya ili hawa viongozi wasimamie na kusiwe na kuwalazimisha wakulima kulipia hizo mbegu,” alisema Bashe.
Kwa upande wao baadhi ya wanunuzi wa zao la pamba walisema watahakikisha wanalipa haraka iwezekanavyo deni la wakulima ili waweze kuingia msimu mwingine wa kilimo na kusambaza mbegu kwa wakulima.
Mmoja wa wanunuzi hao, Fred Shoo alisema wakilipa mapema watapata fursa ya kujiandaa kwa msimu unaofuata, huku akiishukuru Serikali kwa kuwa na usikivu katika kuratibu mazingira ya biashara ili yalete faida kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema kikao kimeazimia madeni yote ya mwaka jana yalipwe kabla ya Desemba 8, ili iwe chachu ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa msimu ujao.
mwisho