Na Brighiter Masaki
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amekasirishwa na utaratibu usiofaa wa ukamataji magari kwenye maegesho yasiyo rasmi.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi kwenye Jengo la Utawala la Manispaa ya Ubungo, Makalla, ameipongeza manispaa hiyo kwa usimamizi mzuri wa fedha za Serikali na kuwataka watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.
Makalla ameelekeza kuitishwa kikao cha dharura baina yake, Wakurugenzi wa Halmashauri na TARURA ili kupatia ufumbuzi, Makalla amefikia hatua hiyo baada ya kupokea Malalamiko mengi ya Wananchi.
“Wananchi wanalalamika juu ya utaratibu mbovu unaotumika na kama kiongozi siwezi kuruhusu jambo hilo liendelee.
“Baadhi ya vijana wanaofanya kazi hiyo wamekosa weledi na busara na wengi wao wamekuwa wakivizia mtu afanye kosa ili wamuadhibu badala ya kutoa elimu ili makosa yasifanyike.” amesema Makalla
Hata hivyo Makalla ameipongeza manispaa hiyo kwa ukusanyaji mapato hali iliyosababisha waanze kutekeleza miradi kwa fedha za ndani na pia kutumia Force Akaunti kukamilisha miradi iliyokuwa ikisuasua ikiwemo jengo hilo la utawala.