PARIS, UFARANSA
RAIS Emmanuel Macron wa Ufaransa amewaomba viongozi wa dunia kupinga kile alichokitaja sheria ya ‘mwenye nguvu kuliko wote mpishe’.
Macron alikuwa akikosoa vikali mtizamo wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kushughulikia kivyake changamoto zinazoikumba dunia.
Macron hakumtaja kwa jina Trump, lakini hotuba yake ya juzi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alianisha misimamo ambayo ni tofauti kabisa na mtizamo alionao rais huyo wa Marekani.
Macron alisema, “baadhi ya viongozi wameamua kufuata sheria ya mwenye nguvu mpishe. Lakini hilo haliwezi kumlinda yeyote, badala yake naunga mkono ushirikiano na mashauriano yanayoshirikisha pande zote kama msingi wa Umoja wa Mataifa na juhudi za kufikiwa amani duniani.”
Kiongozi huyo wa Ufaransa pia amesema kuongezeka kwa ukosefu wa usawa wa kiuchumi ni moja ya vichocheo vya mizozo huku takriban watu milioni 783 duniani wakiishi katika umasikini na watoto milioni 250 wakikosa elimu.