Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, ametembelea Karikaoo , jijini Dar es Salaam jana Novemba 3, 2021 kwa lengo la kuangalia namna bora ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga kutumia majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanyia biashara.
Hatua hiyo imetokana na wafanyabiashara hao kuandika barua Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuomba kupatiwa sehemu za kufanyia biashara katika majengo ya NHC yaliyopo Kariakoo baada ya Serikali kuwaondoa maeneo ya barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ombi la wafanyabiashara hao liliifanya TAMISEMI kuiomba wizara hiyo kuangalia namna ya kuwasaidia wamachinga kwa kuwapatia sehemu kwenye baadhi ya majengo ya NHC yaliyopo Kariakoo ili waweze kufanya biashara.
Imesema kutokana na NHC kuwa chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na maombi ya TAMISEMI, imemfanya Dk. Mabula kuamua kufanya ziara ya kukagua majengo yaliyoainishwa kwenye mitaa ya Tandamti na Msimbazi kwa ajili ya kujiridhisha na kuona kama yanaweza kufaa kwa biashara za wamachinga.
“Hata hivyo, majengo ya NHC yaliyoainisha katika mtaa wa Msimbazi na Tandamti yameonekana hayakidhi vigezo lakini Naibu Waziri wa Ardhi na timu ya viongozi wa NHC walibaini majengo mengine matatu yatakayofaa kwa shughuli za wamachinga.
“Akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uendelezaji Biashara wa NHC, William Genya, Kamishna wa Ardhi Msaidzi Mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kayera na Meneja wa NHC Mkoa wa Ilala Erasto Chilambo,Dk Mabula alitembelea majengo kadhaa na kuridhia majengo matatu yaliyopo mtaa wa Mkunguni na Nyamwezi na kusema yanaweza kuboreshwa na kutumika.