Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
MABONDIA wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Ismail Galiatano na George Bonabucha wanatarajiwa kuwa miongoni mwa wataopanda ulingoni Oktoba 30, mwaka huu katika pambano la ‘Dar Boxing Derby lililpewa jina la Usiku wa Mwana Ukome.
Katika usiku huo ambao mapambano makubwa yatakuwa kati Francis Miyeyusho na Adam Kipenda, Idd Pialali akizichapa dhidi ya Ramadhan Shauri kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
Kwa upande wa Galiatano atapigana na Allan Kamote, wakati Bonabucha atazichapa Haji Juma wote wakitokea Tanga.
Akizungumzia pambano hilo, Galiatano amesema mashabiki wake watarajie mchezo mzuri na hana shaka na mpinzani wake kutokana na mazoezi anayofanya.
“Nimejiandaa vyema, naamini yoyote atakuja atafurahia kwa sababu nitamchezesha mpinzani wangu vile ninavyotaka mimi,” ametamba Galiatano.
Naye Bonabucha amesema mpinzani wake ajiandae kupata kichapo ikiwezekana atamaliza mchezo mapema kwa K.O.