Na Peter Fabian, MWANZA
MIRADI miwili ya majisafi inayosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeshindwa kukamilika kwa muda mrefu sasa kutokana na ubovu wa mabomba na viunganishi vyake, imefahamika.
Habari zinasema hali hiyo imekuwa ni mateso kwa wananchi wa Kata ya Kayenze wilayani Ilemela na Fumagila, Kata ya Kishiri Wilaya ya Nyamagana, ikizingatiwa imegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.6.
“Katika mradi wa Kayenze vifaa viko chini ya kiwango na taarifa zinaonyesha fedha iliyotumika kununulia vifaa hivyo ni zaidi ya Sh milioni 800.
“Vilevile mkandarasi wa kazi hii hajulikani lakini Halmashauri ya Jiji la Mwanza ndiyo msimamizi.
“Mradi ulianza mwaka 2011 hadi leo ni miaka mitano majisafi hayajatoka kwa wananchi hili ni jipu,” kilieleza chanzo chetu za habari.
Alisema kwa mradi wa Fumagila-Kishiri (Nyamagana) wataalamu wamekuwa wakidai uko kwenye majaribio ya mwisho ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema tatizo ni lilelile la ununuzi wa vifaa vilivyo chini ya kiwango vya thamani zaidi ya Sh milioni 700 kiasi kushindwa kutoa maji.
Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM) amekuwa akiwaomba wataalamu wa halmashauri kukamilisha mradi huo bila mafanikio.
“Fedha ya serikali iliyotolewa na Wizara ya Maji imetafunwa kwa kununuliwa vifaa vilivyo chini ya kiwango… maji yakifunguliwa maji tu mabomba yote yanapasuka,” alisema Mbunge huyo.
Baadhi ya wananchi wa Fumagila wametaka hatua kali zichukuliwe kwa wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutokana na mradi huo kushindwa kutoa huduma kwa muda mrefu.
Naye Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire amemtaka Mkurugenzi wa Jiji hilo, Kiomoni Kibamba kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa kuwa fedha zilikwisha kutolewa na Wizara ya Maji.