24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

MABIFU 3 YALIYOTINGISHA 2016

diamond-kiba

Na JOSEPH SHALUWA

BIFU ni kirusi hatari kwa wasanii duniani. Kwa bahati mbaya inatanabaishwa kuwa, wakati fulani (ingawa kwa asilimia ndogo sana) bifu husaidia kukuza sanaa na wasanii husika kwa jumla.

Hapa Bongo, wapo wasanii kadhaa ambao wamejikuta  wakiingia kwenye bifu na wasanii wenzao kwa sababu mbalimbali.

Listi ni ndefu lakini kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mastaa Wema Sepetu na Nasibu Abdul ‘Diamond’ ndiyo wanaoongoza kwa kuwa kwenye mabifu yanayofuatiliwa zaidi.

Wema mpaka sasa hazungumzi na Kajala Masanja. Kuna wakati Wema alikuwa hapikiki chungu kimoja na Aunt Ezekiel lakini kwa sasa wameshayamaliza.

Mpaka ninapoandika makala haya, Wema hayupo sawa na Muna.

Achana na bifu la Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Hamisa Mobeto, ipo listi ndefu sana ya wasanii wenye mabifu.

Kwa sababu tunaelekea mwishoni mwa mwaka, Swaggaz inakuletea mabifu matatu yaliyofuatiliwa zaidi.

 

GARDNER, JIDE

Mei, mwaka huu, mtangazaji bei mbaya Bongo, Gardner G. Habash akiwa katika ukumbi mmoja wa starehe usiku, alitamka maneno yasiyo na staha akiyalenga kwa mtalaka wake, mwanamuziki Judith Wambura ‘Jide’.

Jide na Gardner baada ya kuachana, kila mmoja alishika hamsini zake, bila kurushiana maneno, lakini team zao kwa nyakati tofauti zilionekana kuchochea uhasama kati yao.

Tetesi zilizopatikana baadaye zilisema kuwa, Gardner alikuwa akimjibu Jide baada ya kuachia kibao chake cha Ndi Ndi Ndi ambacho kwa sehemu kubwa kinaonekana kulenga kumrushia vijembe.

Katika kile kilichoonekana kumrusha roho Jide, baadaye zilisambaa picha zinazowaonyesha Gardner na  Giggy Money wakiwa kwenye mapozi yaliyoacha viulizo.

Hata hivyo, Jide katika mahojiano na  Swaggaz yaliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff, Masaki jijini Dar es Salaam, alikataa kuongelea chochote kuhusiana na ishu yake na Gardner kwa maelezo kuwa, walikuwa wameshatalikiana na hivyo haoni sababu ya kuongelea chochote.

 

JIDE AJIBU MAPIGO

Baada ya kimya cha miezi takribani mitano, Jide aliibuka na kusambaza picha zikimwonyesha akiwa na mwanaume aliyemtambulisha kama mume wake.

Akitundika picha na kuandika maelezo katika mtandao wa Instagram, Jide aliishukuru kampuni ya ndege waliyotumia kusafiria na ‘mumewe’ huyo kwenda Zanzibar kwa ajili ya fungate lao.

Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa, haikuwa ndoa halisi, bali ni sehemu ya picha za video ya singo yake mpya. Wapekupeku wa mjini wanaeleza kuwa, hatua ya Jide kufanya hivyo, pamoja na kwamba alikuwa na lengo la kuipa kiki video yake hiyo, alifanya hivyo ili kumrusha roho mtalaka wake Gardner.

DIAMOND, ALI KIBA

Hawa bifu lao ni la muda mrefu sasa, ingawa habari za chini ya kapeti zinasema kuwa ni bifu la kutengeneza wakiwa na nia ya kupata kiki ya kazi zao. Tangu mwaka 2014 katika ujio wa Mfalme Kiba, bifu hili limeunguruma mpaka sasa.

Pamoja na kuwa na uhai mrefu, bado ndilo bifu linalosemwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Kitu kikubwa ambacho mpaka sasa hakijafutika vichwani mwa wapenda burudani Bongo, ni kitendo cha Kiba kumtaja meneja wa Diamond, Sallam SK kuhusika na hujuma ya kuzimwa kipaza sauti wakati akipafomu kwenye shoo ya Mombasa Rock Music Festival, jijini Mombasa, Oktoba 8, mwaka huu katika Viwanja vya Mombasa Golf Club.

Yalitembea maneno mengi, lakini hivi karibuni Diamond katika kibao chake akiwa amefanya kolabo na Rich Mavoko kiitwacho Kokoro, katikati ya video ya singo hiyo ameonekana kumjibu Kiba.

Katika video hiyo, kuna mahali wakifika katikati, kunaonekana kama kukatika kwa picha na sauti, kisha sauti inasikika: “Aaaah! Atakuwa Sallam nini?!”

OMMY DIMPOZ, DIAMOND

Hili ndiyo bifu la fungamwaka. Hawa walitokea kuwa marafiki wakubwa, kukapita kimya cha muda, sasa wamegeuka maadui wakubwa.

Bifu la hawa majamaa ambao wanatambiana muziki mzuri, mashabiki na ujanja kwenye game limefikia pabaya kiasi cha kufikia hatua ya Diamond kuzungumzia kwa kirefu kwenye redio moja ya burudani Bongo, akipangua tuhuma zilizotolewa na Dimpoz ikiwemo ile ya kununua viewers kwenye mtandao wa Youtube.

Baadaye Dimpoz naye alialikwa kwenye kipindi na kufunguka mambo kadhaa kuhusiana na muziki wake na bifu lake na Diamond.

KUTOKA SWAGGAZ

Sisi hatuamini katika bifu, lakini ikiwa wasanii hawa na wengine waliopo kwenye mabifu ni ya kutengeneza kwa lengo la kujipandisha chati na iwe hivyo.

Lakini kama ni uhasama na ugomvi, ni rai yetu kwamba meza ya mazungumzo ni nzuri zaidi kwao ili kuondoa tofauti hizo. – Mhariri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles