MKURUGENZI wa Kituo cha Taaluma ya Mabadiliko ya Tabianchi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Pius Nyanda, amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha idadi ya samaki kuendelea kupungua baharini.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipotoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi ulioandaliwa na UDSM na unatarajiwa kufunguliwa wiki ijayo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
“Mfano kwa ukanda wa bahari sasa hivi kuna kuongezeka kwa kina na joto la bahari na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya viumbe wakiwamo samaki wanaoshindwa kuendana na mabadiliko hayo,” alisema Profesa Nyanda.
Alitaja athari nyingine kuwa ni maji ya bahari kuingia katika mashamba ya kilimo, visima vya maji na katika maeneo ya makazi.
Kuhusu ukame na mvua alisema hautabiriki na hivyo kuathiri kilimo kinachofanywa maeneo hayo.
“Zamani mvua zilikuwa zinatabirika lakini sasa hivi mkulima anapanda mbegu kwa kubahatisha kwa sababu mvua hazitabiriki tena,” alisema Profesa Nyanda.
Kwa nyanda za juu, alisema athari zilizopo ni kuongezeka kwa kiasi cha mvua na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo na kuuhamisha wenye rutuba na kuwalazimisha wakulima kulazimika kutumia mbolea nyingi.
Kutokana na hali hiyo, alisema wao kama wanasayansi ukomo wa kazi yao unaishia katika kutoa taarifa za kisayansi ili ziweze kutumiwa na vyombo vya utekelezaji.
“Wanasayansi tuna jukumu la kufanya utafiti na kutoa taarifa ili ziweze kutumiwa na watunga sera, watu wa mipango na watekelezaji wa ngazi za chini,” alisema Profesa Nyanda.
Kuhusu mkutano huo, alisema unatarajiwa kuanza Oktoba 31 hadi Novemba 4, mwaka huu na Samia atazindua kitabu kinachohusu ufugaji wa asili na athari za mabadiliko ya tabianchi kilichoandaliwa na UDSM.
Pia alisema mkutano huo utawakutanisha watafiti, watunga sera, watu wa mipango na watekelezaji wa ngazi za chini ili kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali zinazohusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake.