Dar es Salaam
WAKATI suala la madai ya polisi kusaidia wafanyabiashara kutorosha dhahabu ya mabilioni likiwa halijafutika kwenye vichwa vya wananchi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana, amerudishwa makao makuu ya polisi Dar es Salaam.
Taarifa ya polisi iliyotolewa jana, ilisema Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amefanya mabadiliko hayo ambayo ni ya kawaida ya utendaji kwa jeshi la polisi.
Hata hivyo kwa uamuzi huo, ni rahisi mabadiliko hayo yakahusishwa na suala hilo la dhahabu kwa vile kwa siku za karibuni mabadiliko kama hayo yamekuwa yakifanywa kunapotakiwa kupisha upelelezi wa jambo fulani.
Januari 22, IGP Sirro aliwarejesha makao makuu ya polisi, makamanda watatu wa polisi baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kuwatupia tuhuma mbalimbali na kutangaza kuwa amewafuta nafasi zao hizo.
Kauli ya Kangi ilizua mvutano kama alikuwa na mamlaka hayo, na makamanda hao wa mikoa mitatu ya polisi waliendelea kubaki ofisini hadi IGP Sirro, alipotangaza kuwarudisha makao makuu ya polisi kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizowakabili.
Makamanda hao na mikoa yao kwenye mabano ni Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhan Ng’anzi (Arusha), Kamishna Msaidizi, Emmanuel Lukula (Temeke) na Kamishna Msaidizi, Salum Rashid (Ilala).
Lakini taarifa ya jana ilisema makamanda walioguswa na mabadiliko hayo yaliyosemwa ni ya kawaida, ni Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Mussa Taibu, anayekuwa kamanda wa polisi Kinondoni.
Aliyekuwa kuwa Kamanda wa Polisi Kinondoni, Muliro Jumanne anaenda kuwa Kamanda wa Polisi Mwanza kuchukua nafasi ya Shana.
Suala la dhahabu
Akizungumza Januari 9, Rais John Magufuli alimpongeza IGP Sirro kwa kufanikisha kukamatwa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Rais alisema uimara wa kiongozi huyo ndiyo ulifanikishwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao na askari waliotaka kufanikisha utoroshaji huo.
Alisema alikuwa na taarifa za kutosha kuwa askari waliowakamata wahalifu hao walikula njama na kutaka kuwasaidia kutoroka baada ya kuahidiwa Sh bilioni moja.
“Mie ninashangaa watu wanaongea vitu wasivyovijua, nina taarifa za kutosha na katika hili nimpongeze sana IGP alisimama kidete kuhakikisha wote wanakamatwa na dhahabu ile inapatikana.
“Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30 zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote,” alisema.
Alisema alikuwa na taarifa za kutosha kuwa askari waliodai kuwafuatilia wahalifu hao nao walikuwa sehemu ya uhalifu
“Watuhumiwa walikamatwa tarehe 4 Misungwi (Mwanza), wakarudishwa mjini na kikosi cha polisi kilichoongozwa na Superintendent.
“Walipoona wamewashika na mali ile wakawapeleka kituo cha polisi lakini hawakuwaingiza ndani wakakaa kwenye gari wakawa wanafanya majadiliano jinsi ya kuwahonga.
“Askari waliahidiwa Sh bilioni moja na wakapewa Sh milioni 700. Wakaondoka nao hadi kwenye Kivuko Kamanga wakawa wanawasindikiza wale wahalifu kwenda Sengerema kwa ajili ya kuwapatia Sh milioni 300 iliyosalia,” alisema.
Alisema kundi hilo likiwa njinia taarifa zikamfikia Kamanda wa Polisi Mkoa na mawasiliano yakafanyika hadi kumfikia yeye aliyeagiza wakamatwe.
Rais Magufuli alisema walipofika mbele walikuta kizuizi cha polisi wakasimamishwa ndipo gari la polisi lililokuwa nyuma likapiga king’ora na kudai walikuwa wakiwafuatilia.
Alisema aliagiza polisi hao wakamatwe na kunyang’anywa silaha kisha wakafungwa pingu na kurudishwa Mwanza kwa hatua zaidi.