26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Mambo matatu yaliyotikisa kampeni Uchaguzi Mkuu Nigeria

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HATIMAYE  ni siku kumi pekee zilizobaki kabla ya wananchi wa Nigeria kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu, nafasi mbalimbali zikigombewa, ikiwamo ile nyeti ya Urais.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo (INEC), watu zaidi ya 80,000,000 wanatarajiwa kupiga kura, vyama vya siasa 91 vitashiriki ma wagombea 72 watakiwania kiti cha urais.

Kupitia Chama chake cha All Progressives Congress (APC), Rais Muhammadu Buhari atagombea kuiwania  awamu yake ya pili Ikulu baada ya ushindi uliomuingiza madarakani mwaka 2015.

Kwa ushindi wake wa kura zaidi ya milioni 15.4 dhidi ya milioni 12 alizokuwa nazo Goodluck Jonathan wa kilichokuwa chama tawala, People’s Democratic Party (PDP), Buhari alikuwa mpinzani wa kwanza kuingia Ikulu.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Februari 16, kampeni za wagombea urais zilionekana kutawaliwa na mambo matatu haya.

Rushwa haikubaliki

Licha ya juhudi za hapa na pale, bado vitendo vya rushwa ni sehemu ya Nigeria kwa muda mrefu sasa. Mwaka 2012, Nigeria ilitajwa kupoteza zaidi ya dola za Marekani bilioni 400 kutokana na rushwa.

Mbaya zaidi, viongozi wa Serikali nao wanatajwa kuhusika, kama ambavyo vyama vya upinzani vimekuwa vikiwanyooshea kidole viongozi wa Buhari wanaotajwa ‘kunanuka’ rushwa.

Akiitumia hiyo kama kete ya kuombea kura, Buhari alisema: “Tumejipanga kumalizia kazi tuliyoianza katika awamu ya kwanza. Lazima rasilimali za taifa ziwekwe katika mazingira ya kumfaidisha kila mmoja,”

Akizungumzia hilo la rushwa, mgombea urais kupitia chama cha Nigeria Community Movement Party (NCMP), Babatunde Ademola, alisema “NCMP itakomesha rushwa, tumejipanga kukabiliana na rushwa katika maeneo yote.

“Rushwa inaweza kukomeshwa ipasavyo endapo tu maisha ya Wanigeria yatafanywa kuwa mazuri. Hii itawazuia watu kuingia katika vitendo hivyo,”

Donald Duke, mgombea wa kiti cha urais kupitia Social Democratic Party (SDP), anaamini kuitokomeza kabisa rushwa ni jambo lisilowezekana lakini Nigeria yake haitajivunia uchafu huo.

“Hata China, ambayo inaendeshwa kwa misingi ya ujamaa kabisa, haijaweza kufanikiwa katika hilo. Rushwa ni kama maisha ya mwanadamu, haitofautiani na kudanganya. Tutahakikisha haifurukuti na si kuiondoa moja kwa moja,” alisema.

Kuinua uchumi

Kama yalivyo mataifa mengi barani Afrika, asilimia kubwa ya wananchi wa Nigeria wanaishi maisha duni, licha ya utajiri wa rasilimali walionao, nikitolea mfano mafuta tu.

Huku Nigeria ikiwa ndiyo nchi inayosafirisha nishati hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi duniani, janga la wasio na ajira limeendelea kuwa changamoto na hata ripoti ya Benki ya Dunia ililiona hilo, ikiitaja kuwa na umaskini wa asilimia 70.

Hali imekuwa mbaya zaidi tangu Buhari alipochaguliwa kuwa Rais kwani alikuta kiwango cha wasio na ajira kikiwa asilimia 10.4 lakini hadi kufikia mwaka jana, tayari ilishafika asilimia 23.1.

Kulikazia hilo, Juni mwaka jana, Shirika la Utangazaji la CNN liliripoti kuwa Nigeria imeizidi India katika orodha ya mataifa yenye idadi kubwa ya watu maskini.

Mpinzani mkuu wa Buhari katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambaye anatokea chama cha PDP, Atiku Abubakar, alisema uongozi wa Buhari ulishindwa kuufanya uchumi wa Nigeria uwanufaishe walio wengi.

“Kama maisha ya Mnigeria yameshindwa kuimarika ndani ya miaka mitatu na nusu, unataka nini tena? alihoji Atiku baada ya Buhari kuomba nafasi ya kurudi Ikulu.

Atiku, ambaye anatajwa kuwapa ajira watu wapatao 300,000 kutokana na biashara zake, anaamini njia sahihi ya kuufufua uchumi wa Nigeria ni kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana wanaoshinda vijiweni, wengine wakiwa na elimu kubwa.

Alisema atataka uwekezaji katika sekta ya mafuta na ubinafsishaji  wa viwanda vya maliasili hiyo  vinavyoshikiliwa na Serikali, huku vikiwa havina  faida yoyote kwa wananchi zaidi ya kuwanufaisha ‘wapigaji’.

Kwa upande wake, Donald Duke wa SDP alisema atahakikisha Serikali yake inakumbukwa katika sekta ya uchumi.

“Ni kwa kupunguza riba na kupigania uwekezaji katika vyanzo vyote vya nishati,” alisema Duke na kuongeza kuwa amepanga kuitolea macho zaidi  nishati ya gesi, akiamini ni fursa kubwa kwa vijana kupata ajira.

Naye  Mchungaji  Habu Aminchi anayeitaka nafasi ya kuiongoza Nigeria kupitia The Peoples Democratic Movement (PDM), aliongezea  akisema inashangaza kuona uchumi wa Nigeria ukizidiwa na Ghana, jambo ambalo halikuwapo huko nyuma.

“Tunataka nchi ambayo itakuwa mahala pazuri kwa wote. Nchi itakayokuwa fahari ya watoto wetu na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Wakati huo huo, Yahaya Ndu wa African Renaissance Party (ARP) alisema anakwenda Ikulu kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi. “Nigeria inapaswa kuwa nchi ya viwanda yenye uwezo wa kutengeneza magari, ndege nanadhalika.  Nigeria inatakiwa kuwa wasafirishaji wakubwa wa bidhaa za kiteknolojia,” alisisitiza.

Boko Haram

Kama kuna jambo linalomchafua Buhari kwa sasa, basi ni usumbufu wanaoupata Wanigeria kutoka kwa Kikundi cha Boko Haram. Wananchi wanapompima kiongozi wao huyo katika suala nyeti la ulinzi na usalama, wanamuona ni aliyefeli.

Bado Boko Haram wameendelea kutesa kwa kipindi chote alichokaa madarakani licha ya ahadi zake za mara kwa mara kuwa atawasambaratisha kwenye uso wa dunia.

Ni hivi karibuni tu, Serikali ya Marekani imewataka raia wake waishio Nigeria kuwa makini kwani huenda magaidi hao wakatumia siku za uchaguzi kutekeleza mashambulio.

Hilo ni angalizo linaloakisi kile kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo Boko Haram walitishia kuuvuruga, kabla ya mashambulio yao katika vituo vya kupiga kura kuondoka na maisha ya watu 41.

Akizungumzia mikakati yake ya kulifyekelea mbali Kundi la Boko Haram endapo atashinda, mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Allied Congress Party of Nigeria (ACPN), ambaye hata hivyo baadaye  alitangaza kujitoa kwenye mbio hizo, Oby Ezekwesili, alisema:

“Serikali yangu itaanza kwa kufumua mfumo mzima wa ulinzi ili kushinda vita dhidi ya Boko Haram. Tunahitaji watu wapya watakaoweza kuondosha tatizo hili,”

Aidha, mwanamama huyo msomi wa Shahada ya Uzamili ya Sheria na Diplomasia, alisisitiza kuwa kuna uwezekano mkubwa watu wanaojiingiza katika masuala hayo ya ugaidi ni wale wasio  na kazi, hivyo Serikali yake italitazama hilo pia.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Elimu huyo wa zamani alisema uongozi wake utahakikisha teknolojia inakuwa ya kiwango cha juu katika shughuli za ulinzi ili kuvirahisishia kazi vyombo vya usalama.

Hilo la usalama lilizungumziwa pia na mgombea urais kupitia SDP, Duke akisema suala la msingi litakuwa ni kukaa meza moja na Boko Haram na kuwashawishi waache uharibifu wanaoufanya.

“Kitakachofuata ni kumaliza umaskini uliopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria (eneo linalosumbuliwa zaidi na Boko Haram). Lile lilikuwa  eneo maarufu kwa kilimo cha pamba.

“Kiwanda cha pamba kilipokufa, watu wakaanza kuwa maskini. Hapo ndipo tatizo la ugaidi lilipoanza,”

Ukiweka kando hilo la Boko Haram, hali ya usalama nchini humo ni mbaya kutokana na machafuko yatokanayo na uhasama mkubwa kati ya wakulima na wafugaji.

Wakosoaji wake wanasema kwa kuwa Buhari ni Mwislamu na anatokea katika Kabila la Fulani, amekuwa kimya kwa kuwa wanaopoteza maisha ni wakulima, ambao ni waumini wa dini ya Kikristo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,608FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles