28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Taharuki yatanda bungeni

Na RAMADHAN HASSA – DODOMA

NI taharuki bungeni. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, kulazimika kuahirisha kikao jana kutokana na  king’ora  cha tahadhari kulia huku wabunge wakipigana vikumbo kutoka nje, kwa mbio.

Tukio hilo   lilitokea jana saa 5.00 asubuhi jijini Dodoma wakati Bunge likielendelea   kwenye kipindi cha maswali na majibu huku Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba akijibu swali la mbunge.

Ghafla hali ya taharuki ilitanda na wabunge wakaanza kutimua mbio   kutoka ndani ya ukumbi.

HALI ILIYOKUWA

Wakati Naibu Waziri Mgumba akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bernadeta Mushashu (CCM), ghafla king’ora cha hali ya hatari kilianza kulia ndani ya ukumbi wa Bunge.

Kuona hivyo baadhi ya wabunge walisimama wasijue ch kufanya huku wengine wakianza kutimua mbio kutoka nje.

Aliyeonekana wa  kwanza kuchukua hatua alikuwa Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), ambaye alitimua mbio ghafla bila kujali kama Bunge lilikuwa linaendelea.

Hatua hiyo iliwazindua  wabunge wengine ambao nao waliamua kufuata nyayo za Mwijage na  kutimia mbio akiwamo  Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF).

 Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, alisimama   haraka na kutangaza kusitishwa   shughuli za Bunge kwa muda.

Mbali na wabunge hao pia wafanyakazi wa Bunge,  maofisa wa usalama  na waandishi wa habari nao walikuwa wakipigana vikumbo   kutafuta njia ya kutoka ndani ya ukumbi huo wa Bunge huku king’ora kikiendelea kulia kwa muda mrefu.

NJE YA BUNGE

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikani (Chadema), alisema hilo ni tukio la kwanza kutokea tangu alipokuwa mbunge.

Alisema pamoja na hali hiyo,    bado vyombo vya ulinzi likiwamo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, vilishindwa kufika kwa wakati kwenye tukio hilo.

“Ninafikiri bado iko haja ya kujipanga vizuri zaidi kwa vyombo vyetu vya uokoaji, haiwezekani tukio kama hili watu wanakuja baada ya dakika 20, kama ni hatari ya moto jengo si wangekuta limeshateketea!

“Lakini pia hata hawa watu wa usalama ambao hili ni jukumu lao nao wanapanda ngazi kwa kunyata kwenye tukio zito kama hili.

“Sasa unajiuliza, je hawa wanaweza kweli kukabiliana na hali hii, kama ni tukio kubwa je ingekuaje?” alisema Lijualikali.

LUSINDE NA BUNDI

Naye Mbunge wa Mtara, Livingstone Lusinde (CCM), alisema   tangu Bunge lilipoanza vikao vyake limeanza na majaribu ya kila aina akiwamo bundi kutua ndani ya ukumbi.

“Unajua tangu tumeanza Bunge kumekuwa na majaribu mengi mno, maana tumeanza na bundi kutua ndani ya ukumbi.

“Hivyo inawezekana bado hajatoka bundi ndani na ndiye aliyeleta hitilafu kwenye nyaya huko juu, kwa kweli tunahitaji maombi haya ya matukio.

“… ndiyo maana mimi baada ya king’ora tu nilikuwa karibu na Mbatia (James, mbunge wa Vunjo), maana huyu ni mtaalamu wa majanga ndiyo maana tumeweza kukimbia na tuko wote pamoja hapa kama unavyotuona,” alisema Lusinde.

Hata hivyo kauli hiyo ya Lusinde, ilipingwa na Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruku (CUF) ambaye alisema  suala la bundi kutua ndani ya ukumbi wa Bunge halihusiani na hitilafu au dharura iliyotokea.

Alisema tukio hilo sasa liwe ni darasa kwa mamlaka za majanga kuona ipo haja ya kuwa tayari wakati wote  dhurura inapotokea.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR Mageuzi), alisema elimu inahitajika zaidi kwa sababu  hakuna aliyejua anatakiwa kutokea wapi.

 “Ninamshauri Spika atupe elimu kuhusiana  na majanga kwa vile  hatuna utayari wa majanga, sasa niambie ingekuwa moto tungefanyaje?” alihoji Mbatia.

Mbunge wa Viti Maalum, Sikudhani Chikambo (CCM), alisema wakati tukio linatokea alikuwa kwenye mgahawa wa Bunge na alipoona wabunge wenzake wanakimbilia nje ilibidi yeye arudi ndani kufuata mkoba wake.

“Niliukumbuka mkoba wangu sikuwa ndani, sikutaka kujua kuna nini nilikuwa nataka tu mkoba wangu maana kulikuwa na vitu vingi mule,” alisema Chikambo huku akicheka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) alisema wabunge walitakiwa kujua linapotokea tatizo wakimbilie wapi  kuokoa maisha yao.

Mbunge wa Songwe, Philip Mlugo(CCM),  alisema uongozi wa Bunge unatakiwa kupongezwa kwa kufunga mifumo ambayo inaonyesha hatari  inayoweza kujitokeza.

“Ni jambo zuri kuwa na mitambo kama ile ambayo kikitokea kitu chochote tunajua tatizo ni nini,”alisema.

POLISI NA KIBARUA

Wakati wabunge waliwa nje ya ukumbi, Jeshi la Polisi lilikuwa na kibarua cha ziada cha kuwatuliza wabunge kwa kuwataka kuwa watulivu wakati watalaamu wakifuatilia kiini cha king’ora hicho cha tahadhari.

Kazi hiyo iliongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto   akisaidiwa na maofisa wengine wa vyombo vya dola.

Wakati Kamanda Muroto  akiendelea na kazi na hiyo liliingia gari la Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, ambako askari wake walishuka na kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuanza kutafuta chanzo cha tatizo kwa   dakika 45.

NDUGAI NA BUNGE

Ilipotimu saa 6:4 mchana kengele ilipigwa   kuitwa  wabunge ndani ya ukumbi   ambako vikao viliendelea kama kawaida.

Baada ya Bunge kurejea, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliongoza kikao hicho na  alianza kwa kutoa pole kwa wabunge kwa  tukio hilo.

Alisema wataalamu walikuwa wanaendelea kulifanyia kazi suala hilo waweze kujua sababu ya king’ora hicho kulia na baada ya kukamilisha kazi hiyo umma utaalezwa.

“Waheshimiwa wabunge poleni sana kwa yaliyotokea, wataalamu wetu wanaendelea kulifanyia kazi tutakapojua sababu ni nini tutaambiana lakini mpaka sasa hakuna sababu ambayo ipo.

“Kipindi cha maswali kimepita hivyo kama kuna swali tutalifanyia utaratibu hapo mbele  tuweze kuokoa muda tunaendelea katika hatua inayofuata… Katibu,” alisema.

TAARIFA YA BUNGE

Ilipofika   jioni jana,  Bunge kupitia Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, lilitoa taarifa kwa kusema kuwa wataalam wake  walifuatilia na kujiridhisha kuwa hakukuwa na tatizo la moto.

“Leo (jana)  tarehe 5 Januari, 2018 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni ,Mwenyekiti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Giga, (Mb) alilazimika kusitisha kwa muda kikao cha bunge baada ya king’ora cha tahadhari chenye kuashiria hatari kupiga kelele.

“Hata hivyo, wataalamu wetu wamefuatilia na kujiridhisha kuwa hakukuwa na tatizo la moto na hivyo Bunge lilirejea na kuendelea na kikao chake kama kawaida.

“Hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa waheshimiwa wabunge, wafanyakazi wa Bunge wala jengo la ukumbi wa Bunge kufuatia taharuki iliyosababishwa na king’ora hicho,” ilieleza taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles