27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Maaskofu, wananchi ‘wamchanachana’ Slaa

mtz1Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

BAADHI ya viongozi wa dini na wananchi wamesema shutuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kuwa baadhi yao walihongwa na Mgombea Urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, ni upuuzi mtupu.

Wamemtaka atoe ushahidi wa madai hayo kwa kutaja majina ya viongozi na kiasi walichohongwa, wakisisitiza kuwa hizo ni siasa za majitaka na kwamba anaifanyia kazi CCM ili apate njia ya kurudi katika chama hicho.
Rais wa TEC azungumza

Akizungumzia shutuma hizo, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amemtaka Dk. Slaa kutoa ushahidi wa madai yake kuwa maaskofu wa kanisa hilo wamehongwa na Edward Lowassa.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu yake ya mkononi, Askofu Niwemugizi alieleza kushangazwa na tuhuma hizo zilizotolewa na Dk. Slaa dhidi ya maaskofu bila uthibitisho.
“Hizo taarifa ndiyo nazisikia kwako, lakini kama kweli amesema hivyo kwa nini hakuweka ushahidi kuanzia majina ya maaskofu hao waliopewa fedha, kiasi na zilikopokelewa. Lakini kwa upande wangu binafsi sijapokea kiasi chochote kutoka kwa mtu yeyote.

Askofu Niwemugizi alimtaka Dk. Slaa kutoa uthibitisho wa maaskofu wa kanisa hilo kupokea fedha kutoka kwa Lowassa waweze kutoa uamuzi.

“Lowassa nimewahi kukutana naye nilimwalika kwenye shule yangu ya seminari kule Biharamulo… shule yenyewe inaitwa Katoke na nilimuweka wazi sababu za kumwalika na sikupokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwake,”alisema askofu huyona kuongeza:

“Athibitishe hilo aonyeshe kiasi cha fedha na majina ya maaskofu, mimi sijapata kiasi chochote labda kama nimetupiwa kwenye akaunti yangu bila mimi kujua lakini nasisitiza atoe ushahidi.”
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekosti, William Mwamalanga alisema kauli za Dk. Slaa zina dalili ya kuleta kisasi fulani.

“Angekuja mapema kabla ya taratibu hizi kuanza tungemwelewa lakini kwa sasa yupo nyuma ya wakati. Kwanza ameonekana amesukumwa afanye aliyofanya na hilo haliwezi kuwabadilisha Watanzania walioamua kutaka mabadiliko,”alisema na kuongeza: “Hotuba yake haina mashiko na taifa halihitaji watu wabinafsi,”alisema Mchungaji Mwamalanga.

Askofu Gwajima azungumza

Naye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kuwa mshenga wa Edward Lowassa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) .

Pia amekana kuhusika kuwarubuni kwa fedha maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki ambao wanadaiwa kumuunga mkono Lowassa katika mbio zake za urais baada ya kuhongwa fedha.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima alisema Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyokuwa imebakia ndani kati ya bunduki ya CCM ili kuwaokoa.

Alisema yote yaliyosemwa na Dk. Slaa ni tuhuma za uongo hivyo wananchi wazipuuze kwa kuwa mwanasiasa huyo anatafuta uungwaji mkono kwa wananchi aelekee CCM.

“Yaani ni uongo kabisa tena uongo mweupe, imedhihirisha wazi kuwa huyu mtu asingefaa kuwa rais. Ni dhahiri ameona akiwasema wanasiasa wenzake watamjibu kwenye majukwaa yao ya siasa, lakini sasa amewasema maaskofu kwa kuwa wao hawana majukwaa.

“Kwa hiyo namshauri hayo mambo ya kuwahusisha maaskofu na uchaguzi aache uongo wa namna hiyo. Nafikiri awaseme wanasiasa wenzake kuzungumzia mambo ya siasa ila kuwahusisha maaskofu si mambo ya busara,” alisema.

Akizungumzia suala la kuwa mshenga wa Lowassa na Chadema, Askofu huyo alisema anafikiri Dk. Slaa ametumwa na waliomtuma, hivyo anawafanyia kazi watu.

“Kwa kawaida inashangaza kwamba kama watu wawili wanagombana, inatakiwa awepo mtu wa kuwaunganisha, ila anaposema maaskofu 34 haileti maana, haiingii akilini… ameingiza Gwajima, Rostam (Aziz) na maaskofu, haeleweki anachozungumza. Lakini ninachosema kuna waliomtuma ni watu ambao anawafanyia kazi.

“Kikubwa ni kwamba baada ya Lowasaa kuchaguliwa kugombea urais kwa Chadema alichukia, alifikiri Lowassa hataendelea kuwa na umaarufu, sasa anaona Lowassa anakwenda, hiyo imemtia hasira anataka kumchafulia Lowassa, ndiyo maana anaongelea Lowassa Lowassa tu.

“Kwa mfano alisema Lowasa angekuja na wabunge wenyeviti wa CCM, ina maana angemkubali Lowassa aje nao, sasa angekuja nao asingekuwa fisadi? Ni swali zuri ila amekwepa kulijibu.

“Nafikiri Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyobakia ndani ya bunduki ya CCM. Natoa wito kwa waumini wangu wafahamu kuwa hizi tuhuma ni za uongo na namsihi huyo daktari asihusishe maaskofu na uongo wake abaki nao mwenyewe,” alisema Askofu Gwajima.

Maoni ya wananchi

Alphonce Boniface ambaye alipiga simu MTANZANIA na kujitambulisha kuwa ni mpiga kura, alisema Dk. Slaa ambaye jana alijitambulisha kuwa ni mtu masikini na anashindia mihogo, awaeleze Watanzania fedha alizotumia kuita waandishi wa habari katika hoteli kubwa ya Serena pamoja na kulipia vipindi vilivyorushwa moja kwa moja vimegharamiwa na nani.

Alisema alichokisema Dk. Slaa ni kukipigia debe Chama Cha Mapinduzi (CCM) na anachokitaka ni kuingia katika kampeni za chama hicho.

“Orodha ya mafisadi aliowataja … ni vema angeenda kushtaki Serikalini/mahakamani ili Lowassa achukuliwe hatua na si kuwaeleza wananchi kwani kufanya hivyo hakuna faida yoyote.

“Tunamtaka Dk. Slaa aache siasa za majitaka aende mahakamani aeleze yale anayoyajua na kutoa ushahidi ili Lowassa apelekwe mahakamani au achukuliwe hatua.

Alisema zipo nchi mbalimbali kama vile Sudan, Kenya na Afrika Kusini ambazo wagombea wao walikuwa na tuhuma za mauaji, ubakaji, kuhodhi ardhi lakini wananchi waliwapenda na kuwapa uongozi na wanafanya vizuri.

“Wananchi tunatakiwa tuamke na tuwe makini kuchagua viongozi ambao wataweza kutatua changamoto zinazotukabili na si kusikiliza siasa za wagombea ambao wanashindwa kutekeleza ahadi zao.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Hombo, Asifiwe George, Gabriel Mushi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles