Renatha Kipaka,Muleba
MKUU wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila,amesema kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI imepungua kutoka asilimia 7.0 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 3.0 Novemba, 2021 kutokana na utoaji wa elimu na uhamasishaji kutumia kinga.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI yaliyofanyika Kiwilaya kwenye Kijiji cha Buhaya, wilayani wilayani humo, Duniani, Nguvila, amesema mbinu zinazotumika ni utoaji wa elimu kwa kutumia Kamati ya Kudhibiti UKIMWI.
“Niwaombe wananchi hasa wanaume tujitokeze kwa wingi kupima afya zetu maana wanawake wamekuwa wakijitokeza kupima afya zao lakini wanaume tumekuwa na mwitikio hafifu na ambao mna maambukizi ya virusi vya UKIMWI hakikisheni mnatumia dawa za kufubaza virusi na kutumia lishe bora ambayo itaimarisha afya zenu,”ameeleza Nguvila.
Amesema ni wajibu wa kila mwananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja kudhibiti maambukizi kwa kuendelea kutoa elimu na hamasa, kwani lengo la Serikali ifikapo mwaka 2030 maambukizi yawe asilimia 0.
Aidha ameagiza wataalamu wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, kuendelea kutoa elimu kwa jamii na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ili wajiunge katika vikundi na kujipatia fedha za mkopo ambayo haina riba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila, amewataka wananchi kutowanyanyapaa waathirika bali wawape kipaumbele wanapokuwa na mahitaji.
Kwa upande wake Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI Wilaya ya Muleba, Henerietha William, amesema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba 2021, waliojitokeza kupima ni watu 71,086, kati ya hao waliokutwa na maambukizi ni 2,273 sawa na asilimia3.0.