KINSHASA, DRC
WIZARA ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema visa vya vifo na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola viliongezeka kwa kasi wiki iliyopita.
Wizara imewatupia lawama waasi kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi na vituo vya afya, ikisema mwenendo huo ni sababu ya ongezeko hilo.
Wizara hiyo imesema kati ya Aprili 22 na Aprili 28, kulikuwa na maambukizi mapya 126 na vifo 83.
Idadi jumla ya vifo imepanda ghafla kutoka 600 mwishoni mwa Machi, hadi 900 mwezi mmoja baadaye.
Takwimu za wizara hiyo mjini Kinshasa zinaonyeha kuwa tangu kutokea mripuko mpya wa Ebola nchini humo mwaka jana, tayari watu 1,480 wamepata maradhi hayo, na 970 miongoni mwao wakiwa wameaga dunia.
Makundi kadhaa yenye silaha yanaendesha shughuli zao mashariki mwa Kongo, na wenyeji wa maeneo yanayokumbwa na Ebola hawana imani na wahudumu katika sekta ya afya.