Shirika la Afya Dunia WHO limetoa taarifa ya mataifa matatu barani Afrika, Algeria, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Nigeria yamebainka kuwa na watu wenye maambukizi ya virusi vya corona kutoka wimbi la nchini India.
Jumla ya mataifa saba ya Afrika yamethibitika kuwa na maambukizi ya aina mpya ya kirusi kutoka nchini india cha B.1.617, ambapo utafiti wa awali unaonesha kuwa aina hiyo ya kirusi kinasambaa haraka kuliko aina nyingine yeyote ya virusi vya corona.
Dkt Ngoy Nsenga kutoka shirika la afya Duniani WHO ambaye anaratibu shughuli za WHO katika kukabiliana na Covid-19 barani Afrika, amesema taarifa zaidi zitatolewa kuhusu watu walioambukizwa au historia ya watu waliosafiri wakiwa wana virusi hivyo nchini Algeria, DRC na Nigeria, .
Mataifa manne ya Afrika tayari yamethibitisha kuwa na aina mpya ya virusi vya corona ambayo inahusisha na wasafiri kutoka India ikiwepo nchi ya Kenya ina watu kumi na tano waliopata maambukizi hayo.
Morocco ina watu wawili, Afrika Kusini ina watu wawili, Uganda ina mtu mmoja wenye maambukizi hayo kutokea nchini india.
Hivi karibuni WHO imesema, kirusi cha India kilianza kuonekana Oktoba 2020, na kuleta hofu duniani.
Kuna utafiti unaosema kuwa wimbi jipya la maambukizi ya corona limeongeza idadi ya vifo nchini India, na sasa hospitali zimejaa huku wakikosa maeneo ya kuzika au kuchoma maiti.