Na Silvan Kiwale, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uko palepale licha ya kujiuzulu uenyekiti kwa Profesa Ibrahim Lipumba.
Kauli hiyo aliitoa jana jioni alipokuwa akizungumza na mamia ya wanachama na wapenzi wa chama hicho waliofurika katika Ofisi za makao maku ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja katika siasa kuna safari ndefu yenye misukosuko ambapo watu wengi watashia njiani lakini yeye bado naamini Watanzania na wana CUF hawezi kurudi nyuma katika harakati za ukombozi wa kweli.
“Ukawa iko palepale, safari hii ni kama ya treni ambayo hubeba mabehewa na abiria wengi ambao ukifika mahali wengine wanashuka na wengine kupanda, kwetu wana CUF tuendelee kuwa na mshikamano katika kipindi hiki.
“Sasa tunajiandaa na vikao vya chama na Jumapili mambo haya yatawekwa sawa kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, namuheshimu sana Profesa Lipumba na ninatambua mchango wake mkubwa sana katika kukijenga chama cha CUF na heshima hiyo itabaki palepale daima,” alisema Maalim.