27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yaitisha kikao cha dharura

jussaNA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi ili kutafuta mwanachama atakayekaimu nafasi ya Profesa Ibrahim Lipumba katika kipindi cha mpito.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Jumapili Agosti 9, mwaka huu ingawa haijaelezwa mahali kitakapofanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa Ladhu, alisema CUF inaheshimu maamuzi ya Profesa Lipumba ya kujiuzulu nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho, kwani ni haki yake kwa mujibu wa katiba yao.
“Bila shaka, Profesa Lipumba amekifanyia kazi kubwa chama chetu katika kipindi cha miaka 16 ambayo alikuwa mwenyekiti, nafasi iliyomfanya awe kiongozi wetu mkuu.
“Kwa nafasi hiyo, ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini, tunaithamini kazi hiyo na tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa ndani ya chama na nchi yetu kwa ujumla. Tunamtakia kila la heri katika mipango yake ya baadaye,” alisema Jussa.
Alisema CUF inaendeshwa kitaasisi, ndiyo maana uamuzi wake wote umekuwa ukifanywa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.
Jussa alisema pamoja na ukweli kwamba kuondoka kwa Profesa Lipumba katika safu ya uongozi kutaacha pengo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, aliwahakikishia wanachama na wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba chama hakitayumba.
Alisema katika historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi, lakini mara zote imeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili na kukabiliana na athari zake.
“Hatuna chembe ya wasiwasi, kwamba hata mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa chama imara zaidi, chama kinawataka wanachama na wapenzi wake kuwa watulivu na wavumilivu, na kusubiri maelekezo ya vikao vya juu vya kitaifa vya chama,” alisema.
Alisema CUF itaendelea na shughuli zake kama kawaida, na pia itashiriki katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao CUF ni moja ya vyama waasisi.
Jussa alisema chama hicho kitatumia nguvu, uwezo, juhudi na maarifa kuhakikisha kwamba kinaulinda umoja huo ambao unaonekana kuwa mwiba kwa CCM.
Vyama vingine vinavyounda Ukawa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.
MWISHO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles