Mwandishi wetu -Zanzibar
JESHI la Polisi Zanzibar, linadaiwa kuzuia kongamano lililoandaliwa na Kamati ya Maridhiano Zanzibar huku likimtoa nje ya ukumbi wa mkutano Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kongamano hilo lililokuwa lifanyike jana katika ukumbi wa Baitulyamin, Malindi kisiwani Unguja, lilikwama dakika chache baada ya polisi kuingia ukumbini na kuondoka na Maalim Seif.
Wanachama wa ACT waliokuwa ukumbini walitangaziwa kuzuiwa kwa kongamano hilo na kutakiwa kuondoka.
Jana jioni kupitia ukurasa wake wa Twitter, Maalim Seif aliandika; “tunawashukuru polisi kwa kitendo chao cha kuingilia kati kongamano letu, kimepelekea kulitangaza kongamano hilo duniani kote.
“Nataka niwaambie wazi kuwa kitendo chao cha leo hakitanirejesha nyuma hata kidogo, bali kimenitia ari zaidi kufichua maovu wanayoyatenda! Zanzibar yenye amani na maridhiano inawezekana!”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedeyoka, alisema polisi hawajavunja kongamano hilo, ila walipata taarifa za mkusanyiko wa watu katika eneo hilo wakati wakiwa kwenye doria za kawaida.
“Tulipofika tulikuta watu na kuwaambia hapa hamtakiwi kuwapo, ambapo pia tulimshauri Maalim Seif kuondoka na alifanya hivyo,” alisema.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alilaani kile alichodai kitendo cha polisi kuzuia kongamano hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Unguja, Zitto alisema kuvunjwa kwa kongamano hilo, na polisi kumtaka Maalim Seif kuondoka ukumbini, ni kinyume na sheria na taratibu.
Katibu wa Kamati ya Habari na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema baada ya kuzuiwa kwa kongamano hilo, polisi walitoka nje ya ukumbi na Maalim Seif ambaye alikwenda nyumbani kwake.
“Ni ajabu kabisa, utaratibu umefuatwa, inakuwaje hadi jambo la ndani linazuiwa, ila ninachotaka kusema ni kwamba baada ya polisi kutoka ukumbini na mshauri wetu wa chama, Maalim Seif, alitoka na kuelekea nyumbani kwake.
“Hayupo kwenye mikono ya polisi na sasa anaendelea na shughuli zake, kongamano hili halikuwa la kisiasa na halikuitishwa na chama chochote ila kamati ya maridhiano ndiyo iliyohusika na viongozi wetu walialikwa kama washiriki wengine,” alisema.