29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF, LIPUMBA WAINGIA VITA HATARI

NA WAANDISHI WETU-DODOMA/DAR ES SALAAM


NI dhahiri sasa kuna hatari ya Chama cha Wananchi (CUF), kuingia vitani kwa kile kinachoelezwa kuibuka kwa vita ya madaraka na kuwania ofisi ya chama hicho.

Hatua hiyo inatokana na pande mbili zinazovutana kujiandaa kwa mapambano kutokana na kile kinachodaiwa kuwania ofisi kuu ya CUF iliyopo Buguruni, Dar es Salaam.

Wakati wabunge wa chama hicho wanaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wakijiandaa kwenda kufanya usafi katika ofisi hizo Jumapili, wanachama wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, wamekuwa wakifanya mazoezi mazito kujihami dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea, alisema katika siku za karibuni ofisi yao imegeuka kuwa genge la wahuni, hivyo kuna uchafu mwingi.

“Aprili 30 mwaka huu siku ya Jumapili, wanachama ambao hatumuungi mkono Lipumba, tutakwenda katika ofisi zetu za Buguruni kwa sababu hivi sasa zimegeuka kuwa genge la wahuni, hivyo kuna uchafu mwingi, tutakwenda kusafisha.

“Tutafanya usafi huo ili ofisi yetu iendelee kuwa safi na wanachama wote watakaojitokeza waje na mifagio na madekio. Tutatoa kila uchafu ili viongozi halali waendelee kufanya kazi,” alisema Mtolea.

Alipoulizwa kwamba hawaoni kufanya hivyo kama kunaweza kuleta uvunjifu wa amani, alisema tukio lolote watakalokutana nalo watalisafisha.

“Sisi tunakwenda kusafisha ofisi yetu kwa sababu tangu Msajili wa Vyama amtambue Lipumba kuwa mwenyekiti, hatujawahi kwenda, hivyo hatuendi pale kwa ajili ya kuvunja amani, bali tunakwenda kusafisha chochote kisichostahili na hata Lipumba ni uchafu. Tunasafisha ili tufanye siasa,” alisema.

Kuhusu mgogoro wao kuwa mahakamani, Mtolea alisema kesi iliyoko mahakamani ni ya kupinga Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kumtambua Lipumba.

“Jaji Mutungi au Mahakama hawajawahi kusema hata siku moja kuwa wanachama hatuna haki kufika pale ofisini, hivyo sisi tunakwenda kufanya usafi.

“Tumejiandaa kwa usafi, tukikutana na uchafu ambao hatukuutarajia tutausafisha,” alisema Mtolea.

Awali, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh, aliunga mkono uamuzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kulaani tukio la baadhi ya waandishi wa habari kupigwa katika mkutano wa CUF.

Alisema bado hawajaona wajibu wa Serikali katika tukio hilo walilofanyiwa waandishi wa habari ambao walikuwa hawana hatia yoyote.

“Tunawapongeza na kuwaunga mkono TEF kwa kulishughulikia suala hili la waandishi wa habari kupigwa, lazima tuhakikishe kuwa waandishi wanafanya kazi kwa uhuru.

“Bado hatujaona wajibu wa Serikali katika hili wakilaani na kuwahakikishia waandishi wa habari kuwa wanafanya kazi zao kwa usalama,” alisema.

Wiki iliyopita, watu wasiofahamika waliovalia kininja wakiwa na bastola, walivamia mkutano wa wanachama wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif na kuanza kuwapiga pamoja na waandishi wa habari waliokuwapo.

 

WAKARIBISHWA

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema kuwa wao wamejiandaa kuwapokea wabunge hao na kueleza mikakati ya kundi hilo la wabunge kufadhiliwa na Chadema, ikiwamo kuhifadhi kundi la watu wanaodaiwa kuwa majambazi.

“Unajua hawa wa ajabu sana. Je, ni nani aliyewaambia ofisi hapa Buguruni ni chafu? Kama wanakuja wabunge wetu tunawakarisha sana kwa mikono miwili. Ila tunajua wanafadhiliwa na Chadema na kundi la majambazi wamelihifadhi eneo la Mbezi kwa Msuguri ili waje wafanye uhalifu hapa, nasi tunawasubiri,” alisema Kambaya.

 

CUF BUGURUNI

Wanachama wa CUF upande wa Profesa Lipumba, juzi hadi majira ya usiku walionekana wakiwa wanafanya mazoezi huku wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa.

MTANZANIA ilishuhudia watu hao wakiwa juu ya jengo la ofisi kuu za chama hicho zilizopo Buguruni wakiendelea na mazoezi, huku mtu aliyetambulika kwa jina moja la Kingwele akiwa mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo.

Majirani waliokuwapo katika jengo hilo, waliliambia MTANZANIA kuwa mafunzo hayo yameanza pindi wabunge na wanachama wa upande wa Maalim Seif walipotangaza kuingia ofisi kuu Buguruni kwa madai ya kufanya usafi katika ofisi hizo.

 

KAULI YA POLISI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alipoulizwa na MTANZANIA kuhusu suala hilo, alisema bado hajapata barua rasmi inayoonyesha wabunge hao watafanya usafi Jumapili.

Hata hivyo, aliahidi kuwa leo atazungumza na waandishi wa habari kulitolea ufafanuzi suala hilo.

“Hatujapata barua rasmi, lakini kesho (leo) nitazungumza na waandishi wa habari kulitolea ufafanuzi suala hilo,” alisema Sirro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles