26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

AROBAINI ZA VYETI FEKI LEO

*JPM kukabidhiwa majina ya WALIOGUSHI

*Zaidi ya watumishi 10,000 roho mkononi


Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

ZA mwizi ni arobaini. Ndivyo unavyoweza kusema, ambapo Rais Dk. John Magufuli, leo anatarajiwa kupokea ripoti ya  uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu ilieleza kuwa ripoti hiyo itakabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki mjini Dodoma.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa ripoti hiyo ni matokeo ya uhakiki ulioendeshwa na Serikali kuanzia Oktoba mwaka jana.

“Rais Dk. Joh  Magufuli, kesho (leo) atapokea taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

 

Ripoti hiyo inatanganguliwa na kauli iliyotolewa bungeni wiki iliyopita na Waziri Kairuki kwamba watumishi wa umma walioshughi vyeti vya elimu wamefikia zaidi ya 10,000.

Hatua hiyo, inatokana na uhakiki uliofanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo imebaini waombaji kazi 39,511 kati yao, 1,951 wana vyeti vya kughushi.

Kuongezeka kwa idadi hiyo kunatokana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni ambaye alisema anasubiri ripoti ya wafanyakazi wa Serikali ambao wamebainika kuwa na vyeti feki.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam, wakati akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema anafahamu idadi ya watumishi wenye vyeti feki ni zaidi ya 9,000 na anaisubiri ripoti hiyo ili aifanyie kazi.

“Kwa hiyo mnaweza mkaona shida zilizopo katika nchi hii, huku wafanyakazi hewa karibu 19,000, wanafunzi hewa ni zaidi ya 56,000, kila mahali unapokwenda ni matatizo, lakini ni lazima niyatatue matatizo kwa sababu mlinichagua kwa ajili hiyo,” alisema Rais Magufuli.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 kwa ofisi yake bungeni wiki iliyopita Waziri Kairuki, alisema baada ya kubainika kwa hali hiyo, wahusika waliondolewa kwenye mchakato, huku vyeti hivyo vikiwasilishwa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria.

“Wahusika waliondolewa katika mchakato pamoja na vyeti hivyo kuchukuliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika,” alisema.

Inaelezwa kuwa sakata hilo la vyeti feki linawagusa pia mabalozi waliopo katika mataifa mbalimbali, wakuu wa wilaya na wakuu mikoa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles