Na Janeth Mushi, Arusha
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema amefurahi kumuona Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) akiwa na afya njema na kusisitiza kuwa ni kiongozi shujaa.
Maalim Seif aliyasema hayo leo nje ya Gereza Kuu la Kisongo, Arusha baada yakuongea na Lema ambaye anashikiliwa mahabusu gerezani hapo.
Aliongeza kuwa kiongozi huyo akitoka gerezani atakuwa ngangari na mwenye ushujaa zaidi na kuwa waliomuweka gerezani wakidhani atavunjika moyo na kuogopa,hawataweza.
"Lema akitoka atakuwa ngangari zaidi kuliko sasa hivi na bado ataendelea na mapambano haya na yumo katika hali ya kishujaa,ushujaa wake umeongezeka na nimepata moyo kuwa yuko katika hali nzuri kiafya na anasubiri uamuzi wa mahakama," alisema Maalim Seif.
Akizungumzia hali ya mgogoro ndani ya Chama hicho,alidai kuwa mgogoro uliopo ndani ya chama hicho siyo kati yake na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa,Profesa Ibrahim Lipumba na kuwa yeye binafsi hana tatizo na Lipumba na kuwa CUF ni chama kimoja ila Lipumba na genge lake ni waasi wa chama.