30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif awavuruga Polisi Zanzibar

Maalim_Seif_SharifNa Mwandishi Wetu, Pemba

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Shei-khan Mohamed, amesema uhalifu unaoendelea mkoani hapo ni matokeo ya ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyoifanya Mei mwaka huu Kisiwani Pemba.

Amesema Jeshi la Polisi linapata changamoto katika kushughulikia kesi za uhalifu huo kutokana na wananchi kugoma kutoa ushahidi kwa sababu wengi ni wanachama wa CUF.

Hayo aliyasema jana visiwani Zanzibar alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika mkutano wa makamanda wa Polisi wa Zanzibar na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni uliofanyika makao makuu ya polisi Zanzibar.

“Matukio ya hujuma yalianza kujitokeza Mkoa wa Kusini Pemba baada ya ziara ya Mei 17 mwaka huu huko Pondeani Jimbo la Mtambile Wilaya ya Mkoani Pemba na ile ya Mei 18 huko Kwale Jimbo la Ziwani Wilaya ya Chakechake Pemba,” alisema na kuongeza:

“Wanachama wa CUF walihamasishwa kufanya migomo na vitendo vingine dhidi ya wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuidhohofisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)”.

Alisema miongoni mwa matukio hayo ni lile la Juni 6, mwaka huu Ziwani Chake ambako Ali Omar Mrisho, alishambuliwa kwa kupigwa ngumi na watu wawili ambao ni Abdallah Mussa Hamad na Mussa Abdalla Said, kumzuia asiingie msikitini kwa sababu ni mfuasi wa CCM.

Kamanda Mohamed alisema tukio jingine ni la kati ya Mei 29 na Juni 8 mwaka huu Mwakunguu Kendwa Mkoani ambako watu wasiojulikana walikata mikarafuu ipatayo 22 yenye thamani ya Sh 700,000 mali ya Sabiha Mohamed Ali ambaye ni Sheha wa Shehia hiyo.

Alitaja tukio jingine kuwa ni la Juni 10, mwaka huu Nanguji Kendwa.
Katika tukio hilo watu wasiojulikana waliketeza kwa moto nusu ya paa la nyumba ya Issa Shehe Othman na kuteketeza mali ya thamani ya Sh milioni tatu.

Alisema Juni 13, mwaka huu huko Michakaini Chake Mkoa wa Kusini Pemba, wanaume wawili wasiojulikana waliteketeza kwa moto paa la makuti la nyumba ya Omar Khamis Bakar na kusababisha hasara ya Sh milioni 1.7.
“Matukio hayo yanaporipotiwa katika vituo vyetu vya polisi timu ya upelelezi Mkoa wa Kusini Pemba wakiongozwa na RPC, RCO, RCIO, OC na CID hufika kwenye maeneo ya matukio hayo kwa kufanya ukaguzi,” alisema na kuongeza:

“Hata hivyo zipo changamoto zinazotukabili katika upelelezi wa mashauri haya ikiwamo wananchi kuwa wagumu kutoa ushahidi kwa vile wengi wao ni wafuasi wa CUF na matukio mengi kutokea wakati wa usiku na sehemu za maporini.”

Alisema pamoja na changamoto hizo Jeshi la Polisi limejipanga kufanya doria kwa miguu na magari mchana na usiku kusambaratisha magenge ya uhalifu.
Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Masauni, alimwagiza Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kushughulikia mara moja kesi ambazo upelelezi umekamilika watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

Akizungumzia biashara haramu ya madawa ya kulevya alisema zipo taarifa za polisi kushiriki katika biashara hiyo na upelelezi unaendelea ili watakaobainika wachukuliwe hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles