-DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kupinga kile alichokiita kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.
Katika barua hiyo aliyoiwasilisha Septemba 27, mwaka huu alikiri kupokea barua ya Msajili na kumpongeza kwa hatua yake ya kufuatilia kwa kina malalamiko yaliyowasilishwa kwake na watu aliowatambua.
Maalim Seif alisema imebainika ofisi ya Msajili imejikita katika kutoa tafsiri ya Katiba ya Chama cha The Civic United Front (CUF) toleo la mwaka 2014 pamoja na tafsiri ya matukio na uamuzi wa vikao vya chama kwa mujibu wa ufahamu wake.
“Tumebaini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa haina mamlaka ya sheria kutoa “Msimamo na Muongozo” kwa chama cha siasa kilichosajiliwa Tanzania.
“Sheria iliyoanzisha ofisi yako, Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258, haikupi mamlaka ya kutoa msimamo na Muongozo. Badala yake unapewa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa.
“Majibu haya yanatokana na ukweli kuwa ofisi yako imewahi kuonywa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam katika shauri la Madai Na. 6 la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela and Another Versus Registrar of Political Parties and Others mbele ya Mheshimiwa Jaji Mihayo,” alisema.
Alisema pamoja na kubaini yaliyomo kwenye maelezo hayo, Baraza Kuu la Uongozi la CUF limesikitishwa na upotoshaji wa makusudi uliofanywa na ofisi ya Msajili kuhusu tafsiri ya vifungu vya Sheria ya Vyama Vya siasa, Sura ya 258 alivyovitaja katika ukurasa wa pili wa taarifa yake fupi ili kujipa mamlaka ya kushughulikia kile ulichokiita mgogoro wa uongozi ndani ya CUF.
“Ukivisoma vifungu hivyo katika sheria tajwa, utabaini kuwa havina kabisa uhusiano na kumpa mamlaka au wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa taifa wa chama na ama kutengua au kubariki uamuzi halali wa vikao halali vya chama chochote.
“Kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba na kutengua barua yake ya kujiuzulu, Baraza Kuu la Uongozi linatambua kuwa Chama cha The Civic United Front (CUF) kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014. Tunapenda utambue kuwa kujiuzulu kwa kiongozi ni wakati wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1).
“Utaratibu uliowekwa na ibara ya 117(2) hauathiri haki ya kiongozi kujiuzulu wakati wowote. Prof. Ibrahim Haruna Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF kuanzia tarehe 5/08/2015 ambayo ni siku aliyoandika barua hiyo na aliutangaza uamuzi wake huo mbele ya vyombo vya habari tarehe 6/8/2015.
“Katika barua yake ya kung’atuka wadhifa wa Mwenyekiti wa CUF. Prof. Lipumba alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya Chama. Prof. Lipumba alikua na mamlaka ya kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu unaitishwa kukubali kujiuzulu kwake lakini hakufanya hivyo.
“Na aliacha ofisi na majukumu ya Mwenyekiti wa CUF kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba ya Chama kwa zaidi ya miezi 10. Kuna msemo ‘you cannot eat a cake and have it’,” alisema.
Alisema pamoja hali hiyo Msajili wa Vyama ameshindwa kueleza jinsi Profesa Lipumba alivyovamia Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa Agosti 21, 2016 akiwa na genge la wahuni ambao siyo wajumbe wala waalikwa wa mkutano huo.
Ateua wakurugenzi
Pamoja na hali hiyo, jana Profesa Ibrahim Lipumba aliteua wakurugenzi wapya watano baada ya kuwang’oa waliokuwapo awali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba aliwataja walioteuliwa kuwa ni Maftah Nachuma kuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Masoud Mhina kuwa Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Zaynab Mndolwa kuwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria.
Wengine ni Jafar Mneke kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi.
Alisema nafasi ya Mkurugenzi wa Mambo ya nje kutoka Zanzibar itatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilika kikao cha dharura cha Baraza la wadhamini kinachotarajiwa kufanyika kesho.
Vilevile, alimteua Salama Masoud kuwa Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho badala ya Fatuma Kalembo ambaye ana matatizo ya afya.