25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Taasisi za umma zadaiwa bil. 1/- bili ya maji

kassim-majaliwaNa MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote za Serikali mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la Sh. bilioni 1.4 zikiwa ni bili zao za maji.

Alitoa agizo hilo jana alipozungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) baada ya kukagua utendaji kazi wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Niletee haraka orodha ya wadaiwa wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma ambao hawajalipa bili zao. Madeni yote ni lazima yalipwe,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma, anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma za jamii   na kukagua miundombinu ya mkoa huo.

Aliutaka uongozi wa DUWASA na watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi au wawekezaji wanaponunua viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze ujenzi mara moja.

“Tumealika wawekezaji, nataka wajenge viwanda na  hoteli hapa Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” aliongeza.

Pia amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, ahakikishe eneo lililo jirani na chanzo hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya uchomaji moto.

“Uchomaji moto uoto wa asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa nchini na halina budi kusimamiwa hadi liishe,” alisisitiza.

Awali Majaliwa alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA,   David Pallangyo ambaye alisema kwamba kuna wananchi wameanza kujenga na kufanya shughuli za  jamii jirani na chanzo hicho cha maji licha ya kuwa walikwishaondolewa zamani.

Kuhusu wadaiwa sugu,   Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za Serikali ndiyo wanaongoza kwa kulimbikiza madeni.

“Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo kubwa na hao tunawamudu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles