NA MAULI MUYENJWA -DAR ES SALAAM
WATANZANIA wamewachangia waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera hivi karibuni kupitia huduma ya M-Pesa, baada ya kuzinduliwa kupitia Kampeni ya uchangiaji ya ‘Red Alert’ inayoendeshwa na Vodacom Tanzania.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Tanzania Foundation, Renatus Rwehikiza, alisema kati ya fedha hizo zilizochangwa baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya uchangiaji wa waathirika wa tetemeko hilo, Sh milioni 99.51 zilitolewa na kampuni hiyo na Sh 490,000 zilichangwa na Watanzania kupitia M-Pesa.
“Kiasi kilichochangwa na wasamaria wema ni shilingi 490,000 na sisi Vodacom tukatoa shilingi milioni 99.51 ambazo zilijumlimshwa na kupatikana shilingi milioni 100 ambazo hundi yake ilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu Septemba 24, mwaka huu na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, baada ya kampeni ya uchangiaji kuhitimishwa,” alisema Rwehikiza.
Alisema awali taasisi yake ilipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao, lakini kwa kuwa Kamati ya Maafa Bukoba ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa ilikuwa na uhitaji wa fedha zaidi, tuliona ni bora tukabidhi fedha.
Pamoja na hali hiyo, alitoa wito kwa Watanzania, mashirika na taasisi mbalimbali nchini kuendelea kujitoa katika kuchangia waathirika wa tukio hilo, badala ya kuiachia Serikali pekee kwani bado uhitaji ni mkubwa.