Ushirikiano wa Tanzania, China katika elimu

0
1009

img-20160831-wa0073Na FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM

HAKUNA urithi bora duniani kwa mtoto kama elimu kwani huwa ni jambo jema na busara pindi unapomtafutia shule nzuri itakayomjengea msingi bora wa maisha.

Imekuwa ikifahamika mara nyingi kuwa mazingira mengi ya shule hasa zile za msingi yamekuwa si rafiki kwa wanafunzi na changamoto hii imekuwa ikizikumba zaidi shule zilizoko chini ya serikali.

Kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele ndivyo pia uwekezaji kwenye sekta hii ya elimu unavyozidi kuchukua nafasi kwani tunashuhudia uwepo wa mabadiliko makubwa nchini hasa katika elimu ya msingi kinyume na miaka kadhaa iliyopita.

Taifa la China ni moja ya mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza kwenye eneo hili la elimu, msukumo wa nchi hiyo kufungamana kwenye elimu imekuwa sababu inayolifanya taifa hilo kuzidi kukua kiuchumi.

Tumeshuhudia mikakati kadha wa kadha ya taifa hilo namna ambavyo limekuwa likitangaza vipaumbele vyake katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kitanzania wanafikia ndoto zao kielimu huku lugha ya kichina ikiwa ni kigezo muhimu.

Katika kuhakikisha kuwa imedhamiria kusaidia changamoto za elimu zinazoikabili Tanzania, serikali hiyo kupitia Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imekamilisha ujenzi wa majengo mapya yaliyojumuhisha madarasa saba, ofisi za walimu, maktaba na vitu vingine muhimu vinavyopaswa kuwa kwenye shule ya kisasa.

Majengo hayo mapya yamejengwa katika Shule ya Msingi Mlimani.

Profesa Zhang Xaozhen ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo, anazitaja sababu za uwekezaji huo ambao ni wa kwanza kufanyika hapa nchini na kuifanya shule hiyo kuwa ya mfano.

Anasema wanataka kuona wanafunzi wa kitanzania wakisoma kwenye mazingira mazuri  yatakayowahamasisha kujifunza vizuri likiwamo lugha ya kichina ambayo ni muhimu kwasasa.

“Ni ukweli ulio wazi kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na serikali ya Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na China, kwa misingi hiyo ndiyo maana tumeona kuwa kuna haja ya kuhakikisha tunawasaidia wanafunzi wa kitanzania kufahamu lugha inayosukuma uchumi wa dunia kwasasa ambayo itatolewa kwenye mazingira bora.

“Licha ya kwamba Tanzania kuna shule nyingi za msingi lakini tumelazimika kuanza na shule ya Mlimani kutokana na kuwapo kwa mahusiano bora baina yetu na chuo achilia mbali urahisi wa kuifikia shule hii,” anasema Profesa Zhang.

Anasema licha ya kwamba shule hiyo ni ya kwanza na ya mfano nchini, pia lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanafikia wanafunzi wengi zaidi nchini ili kuhakikisha wanatambua lugha hiyo ya kichina.

“Tuna mkakati mkubwa wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Tanzania wanaitambua vyema lugha hii na ndiyo maana mradi ujao utakuwa katika Shule ya Msingi ya King David iliyoko mkoani Mtwara. Kule kuna majengo tayari hivyo tutakuwa na kazi ya kutengeneza ratiba za masomo ifikapo mwezi ujao,” anasema.

Akizungumzia mafanikio ya mafunzo hayo ya lugha ya kichina, Profesa Zhang anasema imekuwa na matokeo chanya ikiwamo kuwajenga wanafunzi kujiamini pamoja na kukuza uelewa wao wa lugha ya Kiingereza.

“Tumekuwa tukiwafundisha lugha hiyo kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya tatu na mara baada ya kumaliza tunatoa vyeti ambapo wanaweza kwenda kujiendeleza baadaye.

“Tunashindwa kuwapeleka China kwa sababu bado ni vijana wadogo hivyo hawawezi kujitegemea, lakini natamani kuona somo hili likiingia kwenye mtaala wa elimu wa Tanzania kama ilivyo kwa masomo mengine. Tuna imani kuwa siku za usoni litatiliwa mkazo,” anasema Profesa Zhang.

SHULE MPYA

Anasema licha ya kwamba kila darasa ni mkondo mmoja lakini pia litatumika kufundishia somo la lugha ya kichina katika siku za Jumatano na Jumamosi ili kuwapa hamasa ya kujifunza zaidi wakiwa kwenye mazingira bora.

“Ujenzi wa shule hii umetumia gharama kubwa lakini yote haya ni kutaka kurejesha fadhila zetu kwa jamii inayotuzunguka kwani tumekuwa karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo tunaona ni busara tukiwasaidia kwenye hili.

“Napenda kuwaomba tu wazazi majumbani kuhakikisha kuwa wanawaruhusu watoto wao kusoma somo hili kwa sababu lina faida kedekede na si kama wanavyolichukulia, lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunasaidia wanafunzi wa kitanzania ndio maana kumekuwa na taasisi mbalimbali zinazofundisha lugha ya kichina,” anasema.

MWALIMU MKUU

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Pendo Kujerwa, anasema mpango wa somo la kichina ambao ulianza mwaka juzi umekuwa ukiongeza uelewa mpana wa wanafunzi, kwani wanafunzi wengi wanaosoma masomo ya kichina wamekuwa na uelewa mkubwa zaidi darasani hasa kwenye somo la Kiingereza.

“Hii ni kwa sababu wanafunzi hawa wamekuwa wakitumia lugha ya Kingereza kuwasiliana na wachina, hivyo imeongeza mwamko mkubwa wa uelewa wao darasani ikilinganishwa na wale ambao hawasomi masomo haya.

“Kuna baadhi ya wazazi hawapendi watoto wao wasome kwa madai kuwa watachanganyikiwa na kwasasa tangu kuwapo kwa majengo haya mapya yamefanya shule yetu kuwa ya kisasa.

“Tumepokea maombi mengi ya wazazi wanaotaka kuhamishia watoto wao hapa lakini tunashindwa kuwapokea kwa sababu nafasi zimejaa,” anasema Pendo.

Akizungungumzia shule hiyo mpya, anasema imejengwa na China-Aided Sino Africa Frendship na kutekelezwa na Kampuni ya Fusian Consutruction, itaanza kutumika mwakani kwani kutokana na kutokamilisha mahitaji muhimu.

“Shule hii ina madarasa saba kama kawaida ambapo kila darasa lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45 sawa na mkondo mmoja, hivyo inabidi baadhi ya wanafunzi kusalia kwenye madarasa haya ya zamani ili kuweza kutosheleza wote,” anasema.

Mwalimu Pendo anaongeza kuwa kwa siku za Jumamosi kumekuwapo na changamoto kutoka kwa wazazi ambao wamekuwa wakiwakatalia watoto wao kwa madai kuwa wanapumzika hali inayosababisha kuwa na mahudhurio hafifu.

MWALIMU WA KIINGEREZA

Mwalimu wa somo la Kingereza ambalo linaelezwa kuwa na mafanikio makubwa shuleni hapo, Patrick Kariba, anasema kuna tofauti kubwa ya uelewa kati ya wanafunzi wanaosoma lugha ya kichina na wale wasiosoma.

“Niseme wazi kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa mno kwa wanafunzi wanaopata mafunzo ya kichina, wamekuwa na uelewa mkubwa zaidi darasani ikilinganishwa na wenzao.

“Wapo ambao awali maendeleo yao yalikuwa hayaridhishi kwenye somo hili la Kingereza lakini kwasasa wanafanya vizuri sana mpaka walimu tunafurahi na hii inatokana na kuhudhuria mafunzo haya ya kichina.

“Hivyo mpango huu ni mzuri mno na wa kuigwa kwani unasaidia kuwajengea uwezo vijana katika kuongeza uelewa wao darasani na ndio maana hata wahitimu wa mwaka jana wamefaulu wote kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza,” anasema Kariba.

Kariba pia anatoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa somo la Kingereza linafundishwa kuanzia darasa la kwanza tofauti na ilivyo sasa ambapo linaanza kufundishwa darasa la tatu.

Kwa upande wake Mwalimu Veneranda Assenga ambaye pia ni mwalimu wa somo la Kingereza shuleni hapo, anasema mafanikio ya mafunzo hayo yamekuwa makubwa kwani kila mmoja amekuwa na hamasa ya kujifunza ikiwamo pia walimu wenyewe ambao wamekuwa wakitamani kujua lugha ya kichina.

WANAFUNZI

Happness Komba (13) aambaye ni mhitimu wa darasa la saba shuleni hapo, ni kati ya wanafunzi walionufaika na mpango huo wa lugha ya kichina.

“Kwasasa naweza kuongea kichina hivyo nina matumani hapo baadaye naweza kujiendeleza na kuwa mkalimani jambo ambalo litanisaidia kuendesha maisha yangu.

“Lugha hii pia imenisaidia kwenye masomo yangu darasani na nimeweza kufaulu vizuri somo la Kingereza na kuzungumza ikilinganishwa na awali kabla ya kuanza kujifunza kichina.

“Hivyo naomba wazazi wawaruhusu watoto wao kujifunza lugha hii ambayo kwasasa ndiyo iko kwenye soko la uchumi wa dunia,” anasema Happness.

Naye Lucy Erenest (13) na Zainab Juma (13)  wa darasa la sita shuleni hapo, wanasema hiyo ni fursa na kwamba wanajitahidi kuhakikisha kuwa wanaitumia vyema.

“Tunayafurahia masomo ya lugha ya kichina kwani kadiri unavyoongeza bidii ndivyo unavyoelewa, tunaamini yatakuja kuwa na msaada mkubwa huko mbeleni,” anasema.

Shule hiyo yenye walimu 47 na wanafunzi 963, licha ya kwamba imetoa wanafunzi maarufu kama Mbunge Halima Mdee, Hashim Thabith, Ruge Mutahaba na wengine ambao wamekuwa wakishirikiana kuweka huduma muhimu shuleni hapo ikiwamo ujenzi wa vyoo na mambo mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here