JENNIFER ULLEMBO NA THERESIA GASPER
MKURUGENZI wa benchi la ufundi la klabu ya Yanga, Hans van der Pluijm, jana alifanya utambulisho wa wachezaji kwa kocha mpya, George Lwandamina, katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, siku ya jana ilitumika kwa utambulisho na mazoezi mepesi ya kupasha mwili.
Saleh alisema wachezaji ambao hawakuweza kuripoti jana, wataungana na wenzao waliotangulia katika mazoezi yatakayoanza rasmi leo.
“Leo (jana) ilikuwa ni siku ya utambulisho, Pluijm alikuwa akimtambulisha kocha kwa wachezaji ili wajuane vema.
“Mazoezi yaliyofanyika yalikuwa ni kupasha misuli tu na kuchangamsha mwili, ila programu rasmi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza kesho (leo),” alisema Saleh.
Wachezaji walioripoti mazoezini ni Amis Tambwe, Deusi Kaseke, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Juma Mahadhi, Vincent Andrew ‘Dante’, Haji Mwinyi, Mbuyu Twite, Matheo Antony na Deogratius Munishi ‘Dida’.
Wengine ni Ally Mustafa ‘Barthez’, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Canavaro’ Godfrey Mwashiuya, Said Juma, Pato Ngonyani na Juma Abdul.
Wachezaji ambao wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo leo ni Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Hassan Kessy na Beno Kakolanya, huku Vincent Bossou akiwa bado ana matatizo ya kifamilia.