MAPEMA wiki hii Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hadi kufikia Disemba 30 mwaka huu wale wote ambao hawajaendeleza viwanja vilivyopimwa na serikali kwa ajili ya makazi watanyang’anywa.
Kauli hiyo imepeleka mshtuko kwa baadhi ya watu ambao hawajaendeleza viwanja hibyo.
Miongoni mwa watu waliokumbwa na mshtuko huo ni baadhi ya wajane ambao ni miongoni mwa waliopiga simu chumba hiki cha habari na kueleza kilio chao.
Maelezo ya wajane hao ambayo karibu yote yanashabihiana ni kwamba wakati serikali imepima viwanja hivyo na kuviuzi wenzi wao walikuwepo na mipango ya kuviendeleza pia ilikuwepo.
Mkwamo wa kuviendeleza viwanja hivyo ulianza pale baada ya wenzi zao hao kufariki dunia na kuwaachia mzigo mzito wa si tu kutafuta makazi bali pia kutimiza haki za msingi kwa watoto walioachiwa kama kuwapatia elimu na malazi.
Wanasema shughuli ya kuwapatia elimu na malazi watoto pamoja na wao wenyewe imewafanya wapate wakati mgumu wa kuendeleza viwanja hivyo.
Kwa mfano mama mmoja anasema; wakati mume wake anafariki alimwacha watoto wake wanne wote wakiwa wako shuleni na anasema alitegemea wakifika ngazi ya kwenda vyuo vikuu kidogo angepata ahueni kwa serikali kuwapatia mikopo lakini hali ilikuwa tofauti.
Anasema kwa miaka yote hiyo amekuwa akipambana watoto wake wapate elimu kwa sababu anaamini mafanikio yako ndani yake.
Ni kwa sababu na maelezo hayo pengine sisi tunaona Waziri Lukuvi akalitazama jambo hilo kwa upana kwani siku zote tumekuwa tukiamini kwamba kuwa kiongozi maana yake ni kusaidia kutatua matatizo na si kuyaongeza.
Hatusemi kwamba hatua aliyotangaza Lukuvi ni mbaya hapana, bali kwa baadhi ya watu wenye kesi maalumu kama baadhi ya wajane pengine serikali ni vyema ikawaangalia kwa jicho la kipekee na pengine kuwapa elimu ya namna ya kufikia malengo waliyoyategemea.
Hatudhani watu kama hawa wenye kesi maalum kuwanyang’anya viwanja kama ni kuwasaidia bali kuwarudisha nyuma na pengine kuwapoteza kabisa.
Tunafahamu lengo la serikali yeyote duniani pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha inawapunguzia wananchi wake umaskini kwa kuwapatia maendeleo na ndio msingi hata wa kupima viwanja hivyo na kisha kuwauzia.
Tunaamini jambo hili linawagusa wengi na si tu katika hili la viwanja vilivyopimwa na serikali bali katika maeneo mbalimbali.
Kwa sababu hiyo tunayo imani, serikali kupitia kwa Waziri wake wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lukuvi italiona jambo hili na hata kutafuta njia kusaidia familia hizo na si kuendelea kuziumiza, kwani maumivu ya kuwapatia malazi na kusomesha watoto yanajulikana kwa yeyote yule anayejua hasa maana ya elimu.