SERIKALI imeliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kusitisha ujenzi wa majengo makubwa ya biashara hadi yale yaliyopo yakamilike.
Pia shirika hilo, limezuiliwa kupandisha gharama za pango hadi maelekezo mengine yatakapotolewa na waziri mwenye dhamana.
Akizungumza na wajumbe wa bodi na menejimenti ya shirika hilo mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema uamuzi huo umefikiwa ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza kwa sababu ya kurundikana kwa miradi.
Alisema shirika hilo, lina miradi ya majengo makubwa ya biashara katika miji ya Dar es Salaam na Arusha ambayo yanaendelea kujengwa, ingawa hakufafanua yana gharama kiasi gani.
“Bodi na menejimeti nawaagiza kusitisha ujenzi wa majengo mapya ya biashara, hadi haya yaliyopo yakamilike kwanza…tukifanya hivyo tutakuwa tumeepuka matatizo,’alisema Lukuvi.
Pia Waziri Lukuvi, amepiga marufuku shirika hilo kupandisha kodi za pango kwa nyumba za Serikali bila kumhusisha, baada ya kuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wapangaji.
“Ni marufuku kupandisha kodi kwa wapangaji wa shirika letu,nina taarifa hivi sasa mmepandisha bila kunishirikisha…mimi ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.
“Ninyi wajumbe wa bodi na menejimenti, suala hili lichukulieni kwa uzito, nasema marufuku, kumekuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wapangaji,”alisema Lukuvi.
Alisema shirika hilo limepandisha gharama za upangaji wa kawaida kutoka Sh 200,000 hadi Sh 800,000 kwa mwezi kiwango ambacho alisema ni kikubwa.
“Nawaomba mnapotaka kupandisha gharama hizi mnishirikishe nikiona inafaa au laa nitawaambia, inakuwaje gharama zinapande bila waziri mwenye dhamana kujua?alihoji Waziri Lukuvi.
“Nyumba zilizopo hivi sasa ni za ghali mno kwa Watanzania walio wengi, hivyo wanashindwa kumudu gharama,”alisema Waziri Lukuvi.
Kutokana na hali hiyo, ameitaka bodi na menejimenti kuunda kamati maalumu ambayo itashughulikia rufaa au kero za wapangaji ambao hawariziki na kiwango hicho.
“Naagiza tena ndani ya bodi hii undeni kamati maalumu ya kushughulikia kero za wananchi ambao hawariziki na viwango hivi…namini itakuwa njia sahihi ya kutatua matatizo yenu,”alisema.
Pia Waziri Lukuvi ameitaka bodi na menejimenti ya NHC kuacha mara moja mpango wake wa kutaka kutengeneza mfumo mpya wa shirika.
“Nimeambiwa mnataka kutengeneza mfumo mpya wa shirika hili, nasema acheni,sitaki kusikia mnauzungumzia tena…huu uliopo unatosha, kila mtu arudi kwenye nafasi yake afanye kazi ili shirika lifikie malengo yake,”alisema Waziri Lukuvi.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza shirika hilo lihakikishe linajenga nyumba 50,000 mwaka huu ambazo zitauzwa kwa gharama nafuu kwa wananchi wa kawaida.
“Nyumba mnazojenga zina gharama kubwa, hakikisheni mnajenga 50,000 na kuziuza gharama nafuu ili kila mwananchi wa kawaida aweze kununua. Mimi mkinipa milioni Sh 20 na mashine ya kufyatulia tofali, nawaambia nitajenga nyumba nzuri kabisa.Ni jukumu lenu kujua zitajengwa wapi na lini.Nawapa mwezi mmoja mje na mkakati wa suala hili,”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alisema tayari wamefanya upembuzi yakinifu katika eneo la Luguruni ambako zitajengwa nyumba za gharama nafuu na zitauzwa kwa kati ya Sh milioni 20, 25 hadi 30.