24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

LUKUVI AWACHARUKIA MAOFISA ARDHI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

 

 

Na BENJAMIN MASESE – MWANZA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amechukizwa na uzembe wa maofisa ardhi wa Jiji la Mwanza kwa kushindwa kuandaa hati za wananchi waliomaliza kulipia gharama zote husika.

Pia amemuonya na kumtaka Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, kumwomba radhi kwa kitendo cha kumpatia taarifa za uongo juu ya mpango wa urasimishaji makazi katika jiji hilo, kwamba wananchi hawatoi ushirikiano katika kulipia gharama za upimaji ardhi na hati jambo ambalo si kweli.

Akizungumza na watumishi wa jiji hilo jana, wakati akiwa katika masijala ya kumbukumbu za hati, alishangazwa kushuhudia mafaili mengi ya wananchi wakiwa wamelipa gharama zote, lakini hakuna hatua yoyote iliyofanywa na watumishi wa Idara ya Ardhi.

Mafaili hayo yalionekana kutoshughulikiwa zaidi ya miaka mitano, lakini watumishi wa Idara ya Ardhi wakiwa ofisini bila kuwajibika na alipowahoji walidai hawakuwa na wino wa kompyuta.

“Naona kazi imewashinda hapa Jiji la Mwanza, hiyo si sababu ya kutoandaa hati zaidi ya miaka mitano, haiwezekani maofisa ardhi wateule watatu mko ofisini, kisha mshindwe kuandaa hati kwa wananchi waliotimiza masharti, sasa naanza na nyie, nitawahamishia vijijini au katika wilaya ambazo uwezo wenu unafaa kukaa pale.

“Mmefanya madudu katika kitovu cha jiji, mmeshindwa kuzingatia agizo langu la kukamilisha hati kwa mwezi mmoja baada ya malipo kulipwa na mwananchi, kasi yenu imekuwa ndogo kupindukia, kwa sababu haiwezekani tangu mwaka jana muandae hati 452 badala ya 19,000.

 “Naagiza kufikia Juni 30, mwaka huu naomba hatia hizo 19,000 ziwe zimekamilika na ndiyo mwisho wa urasimishaji makazi katika Jiji la Mwanza, baada ya hapo Serikali itazindua mpango mji wa Jiji la Mwanza,” alisema.

Maofisa ardhi watakaohamishwa ni Salvatory Luboja, Halima Idd na Charles Liberaho na wameelekezwa na Lukuvi waandike maelezo ya aliyesababisha hati kukwama kwa muda huo kabla ya kuhamishwa.

Pia aliwaonya watumishi wa jiji hilo kwa kuwatoza wananchi kodi ya ardhi, huku wakiwaacha wanasiasa wakiwamo wabunge, matajiri na watumishi wa umma wanaodaiwa zaidi ya Sh milioni 500.

Aliwataka kuhakikisha fedha zote zinakusanywa na wakishindwa kulipwa kwa wakati, wachukue hatua za kisheria, ikiwamo za kumpelekea hati hizo ili aweze kuzifikisha kwa Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles