26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

ILO: WAFANYAKAZI MILIONI 2 WANAFARIKI DUNIA KILA MWAKA

 

 

Na Upendo Mosha – Kilimanjaro

WAFANYAKAZI milioni 2.3 wanadaiwa kupoteza maisha kila mwaka katika nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania, kutokana na ajali wanazokutana nazo mahala pa kazi na kutishia usalama wao.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Magnus Minja, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya na Usalama Duniani na kuhuduriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Ulemavu), Jenista Mhagama.

“Pamoja na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika, lakini ni jambo la kushangaza kuwa watu milioni 2.3 kila mwaka duniani wanawake kwa wanaume hupoteza maisha kutokana na kuumia au kupata maradhi kazini, kwa maana nyingine tunaweza kusema mfanyakazi mmoja hupoteza maisha kila baada ya sekunde 15,” alisema.

Minja alisema masuala ya ajali kazini yamekuwa ni mambo ya kawaida na jambo hilo si la kufanyia mzaha, bali ni la kuvalia njuga na kuhakikisha nchi inazuia matukio ya vifo vya wafanyakazi.

Alisema Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuhadhimisha siku hiyo, lakini kumekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa takwimu sahihi za ajali na matukio ya vifo vinavyotokea sehemu za kazi.

“Nchi zote duniani pamoja na hapa kwetu Tanzania zina wajibu wa kutoa taarifa juu ya viwango vya ajali mahala pa kazi, lakini yapo maendeleo kidogo katika suala hili kwenye ngazi za kitaifa na kimataifa katika ukusanyaji wa takwimu na juhudi hizo ni ndogo kwa sababu kuna upungufu wa ukusanyaji wa takwimu na usahihi wa takwimu hizo,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokwa, alisema ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini wanatimiza masharti ya afya na usalama kazini katika shughuli wanazozifanya.

Alisema ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kuanzisha mitaala ya afya na usalama kazini katika vyuo vikuu mbalimbali na shule za msingi na sekondari jambo litakalosaidia kujenga jamii inayoweza kuthamini afya na usalama mahala pa kazi.

 Pia alisema ni vema Serikali ikaweka utaratibu wa kuondoa kemikali zenye sumu na kuhifadhi mazingira ili kuzua athari zake kutokana na kukua kwa sekta ya viwanda.

 “Serikali itekeleze wajibu wake, lakini pia waajiri watekeleze yafuatayo ambayo ni kuanzisha na kuimarisha mipango ya mafunzo juu ya usalama mahala pa kazi kwa wafanyakazi wake, pia wafanye ukaguzi wa mara kwa mara na kuunda kamati za afya sehemu za kazi na kuhakikisha zinaboresha usalama kwa wafanyakazi,” alisema.

Akifunga kilele cha maadhimisho hayo, Jenista, alitoa wito kwa waajiri wote kutoa taarifa za matukio ya ajali, magonjwa na matukio ya hatari yote kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles