Na MWANDISHI WETU -DODOMA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amefuta uamuzi wa viongozi wa Vijiji vya Membe na Mlimwa vilivyopo Kata ya Membe, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wa kumpatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,756 mwekezaji David Mazoya Poli, takribani miaka 10 iliyopita, hali iliyosababisha mgogoro wa ardhi na kuhatarisha amani katika Kata hiyo.
Hali ya sintofahamu iliwagubika wakazi wa Kata hiyo, kwani licha ya kukataa kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo kupitia mikutano mikuu ya vijiji, viongozi wao walimmilikisha mwekezaji huyo ardhi hiyo, ikiwamo ekari 100 alizopewa na Kijiji cha Membe kwa makubaliano kuwa atawajengea Ofisi ya Serikali ya Kijiji, ahadi ambayo hata hivyo hajaitekeleza.
Akizungumza na wakazi wa Kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara jana, Waziri Lukuvi alisema kuwa, amefuta maamuzi yote yaliyofanywa na Serikali za Vijiji hivyo, kwani yalikiuka Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999, inayotoa mamlaka kwa vijiji kumilikisha ardhi isiyozidi ekari 50 tu na si vinginevyo.
“Kuanzia leo nimefuta maamuzi yote yaliyofanywa na viongozi wa vijiji hivi kumpa mwekezaji huyu ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,756, kwani ni kinyume cha Sheria ya Vijiji…hata kama vijiji vitakubali kutoa ardhi kupitia mikutano mikuu ya vijiji, bado maamuzi hayo hayatakuwa halali endapo ardhi inayotolewa itazidi ukubwa wa ekari 50,” alifafanua Waziri Lukuvi.
Alimtaka mwekezaji huyo ambaye alifika katika mkutano huo, kufuata taratibu za kumilikishwa ardhi inayozidi ukubwa wa ekari 50 endapo ana nia ya kuendelea kuwekeza katika kata hiyo, ikiwa ni kuomba ardhi katika vijiji hivyo na endapo vitaridhia, vitapendekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kumilikisha ardhi inayozidi ekari 50 baada ya ardhi hiyo kuhama kutoka katika mamlaka ya vijiji.
Wakazi wa Kata hiyo walimshukuru Waziri Lukuvi kwa uamuzi huo wa Serikali kwa madai kwamba wameteseka kwa kipindi kirefu, ikiwa ni pamoja na kukosa maeneo ya kulima na malisho kwa ajili ya mifugo yao.