MANCHESTER, England
BEKI wa kushoto wa Manchester United, Luke Shaw, amemhoji kocha wake, Jose Mourinho, akitaka kufahamu sababu za kumpumzisha katika mchezo wa robo fainali wa Kombe la England, FA, dhidi ya Brighton.
Katika mchezo huo uliochezwa Machi 17 mwaka huu, Shaw alionekana kutokubaliana na uamuzi wa Mourinho wa kumbadilisha, licha ya kuelezwa sababu ya mabadiliko hayo yalitokana na kucheza chini ya kiwango.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, ndani ya chumba cha kubadilishia nguo Shaw alimhoji Mourinho: “Kwanini kila wakati mimi ndio hutolewa na kulalamikiwa kuhusu kiwango?”
Mourinho alimjibu beki huyo kuwa hakuwa akizuia vya kutosha, ndiyo sababu ya kumpumzisha na nafasi yake kuchukuliwa na Ashley Young.
Tukio hilo la hivi karibuni lilibainisha kupotea kwa maelewano mazuri ya beki huyo na Mourinho.
Mourinho amekuwa na hofu kuhusu kiwango cha Shaw na uwezo wake wa kufuata maagizo anayompa ndani ya uwanjani.
Shaw anahisi kwamba, amekuwa hatendewi haki na Mourinho na vyanzo vya karibu naye vimezungumzia hali yake ya kukata tamaa msimu huu.
Ni mara ya pili ndani wiki mbili kwa wawili hao kukwaruzana. Katika tukio la kwanza, Shaw alitaka uhakika kuhusu uwezekano wa kucheza katika kikosi cha kwanza, baada ya United kushinda mabao 3-2 dhidi ya Crystal Palace.
Mgogoro wa Mourinho na Shaw baada ya mchezo huo ulisababisha shaka mpya kuhusu hatima ya mchezaji huyo, ambaye amebakisha zaidi ya mwaka mmoja kumaliza mkataba wake katika klabu hiyo.
Manchester United inahusishwa kuifukuzia saini ya beki wa kushoto wa Tottenham, Danny Rose na Ryan Sessegnon wa Fulham, beki wa Juventus, Alex Sandro na Kieran Tierney wa Celtic, ili kuchukua nafasi ya Shaw.
Kutofautiana kati ya Mourinho na Shaw ni miongoni mwa mifano ya Mreno huyo kuwa katika hali ya kutoelewana na wachezaji wake, ambao anawahisi hawafanyi vizuri kulingana na maagizo yake katika mchezo.
Miongoni mwa wachezaji hao ni kiungo aliyesajiliwa kwa kuvunja rekodi akitokea Juventus, Paul Pogba, ambaye alikwaruzana na Mourinho katika mchezo dhidi ya Tottenham, uliochezwa mwisho wa Januari, mwaka huu.
Mchezaji huyo haonekani kuelewana na Mourinho, jambo ambalo limefanya kukosekana katika kikosi cha kwanza, ameanza michezo mitatu ya Manchester United kati ya michezo nane tangu aingie kwenye mgogoro.