Na Mwandishi Wetu |
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limewatoa hofu Watanzania na kusema kuwa wataendelea kununua umeme wa Luku kupitia kwa mawakala wao ambao wameunganishwa na Mfumo wa Malipo wa Serikali (Ge-PG).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Meneja Mwandamizi wa TEHAMA wa TANESCO, Demitruce Dashina, amesema kuwa sasa Watanzania watandelea kununu umeme kama awali.
“Kilichoongozeka hapa mawakala wetu wote walitakiwa na sheria kujiunga kwenye mfumo wa malipo wa Serikali na wote wamefanya hivyo. Watanzania wanatakiwa kuendelea kununua umeme bila hofu ya aina yoyote.
“Tangu Desemba mwaka 2017 wateja wote wa mita ambazo si za Luku walishaunganishwa katika mfumo huo wa Ge-PG na wanaendelea kupata umeme. Kwa mita za Luku tangu Februari 7, tuliwaunganisha Benki ya CRDB na NMB na sasa mawakala wengi wameunganishwa ikiwemo kampuni za simu nchini ambao wamekuwa wakiuza umeme kupitia huduma zao kwa wateja wao,” amesema Dashina
Kwa mujibu wa sheria kuanzia Aprili 2, mwaka huu taasisi na idara za Serikali zinatakiwa ziwe zimejiunga na mfumo huo wa malipo kama njia ya kuiwezesha Serikali kujua mapato yake.