Johns Njozi, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema vyombo vya usalama havishughuliki na kutoweka kwa watu bali wanahusika na watu waliotendewa uhalifu.
Lugola ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 6, katika mkutano wake na waandishi wa habari na wakuu wa vyombo vya usalama wakati alipoulizwa kuhusu kutoweka kwa mwandishi wa habari, Azory Gwanda.
“Kuhusiana na watu kutoweka, sisi Wizara ya Mambo ya Ndani hatuingilii uhuru wa ndani wa mtu, huyo ambaye mnasema ametoweka nyumbani kwake sisi hatuhusiki, kwa sababu kuna mwingine anatoweka kutokana na sababu za kimaisha,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Lugola amemtoa kikaoni Kamishna Mkuu wa Magereza kwa kuchelewa kikaoni huku akiahirisha kikao chake na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na kutokuja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano waliopanga kuufanya baada ya mazungumzo na waandishi wa habari na kuwaagiza wakuu wa majeshi wakachukue ilani ndipo warudi kuendelea na kikao.
Lugola pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kumchukulia hatua ya kumshusha cheo Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Leopod Fungu mwenye cheo cha Mrakibu wa Polisi abaki na nyota tatu, kwa kushindwa kujua idadi ya Wajumbe wa Baraza la Usalama Barabarani na kuwa na taarifa za vikao vya baraza hilo.
Wakati huo huo, Lugola pia amemuagiza Mrakibu Mwandamizi wa Kikosi cha Zimamoto Kagera, George Mrutu ashushwe cheo kimoja kutoka alipo sasa kwa kosa la kushindwa kwenda kuzima moto kwenye mabweni ya wanafunzi katika Chuo cha Ufundi na Udereva cha Lake Zone, mkoani Kagera kwa kisingizio cha kukosa gari la zima moto.