29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Loyal friend: Jinsi Rostam Aziz na marehemu Lowassa walivyobaki marafiki hadi mauti yalipomkumba Waziri Mkuu huyo wa zamani

Na Evarist Chahali

Mmoja wa marafiki wa kweli wa Lowassa alikuwa Rostam Aziz. Ndo aliewezesha sio tu kuondoa tofauti kati ya JPM na Lowassa (JPM alimsumbua mno Lowassa hasa kwenye biashara zake) bali pia “kumrudisha nyumbani” CCM. True friends are hard to find ktk chama cha kinafiki kama CCM.

Evarist Chahali (@chahali), Twitter, Februari 13, 2024

Hiyo ilikuwa twiti ya Jasusi akieleza kuhusu moja ya mafunzo muhimu kuhusiana na kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Edward Lowassa aliyefariki Februari 10 na kuzikwa Februari 17.

Twiti hiyo iliakisi ukweli kwamba mtu anayeweza kutajwa kama rafiki wa kweli wa marehemu Lowassa miaka nenda miaka rudi ni mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz.

Urafiki kati ya Rostam na Lowassa ulianzia mbali hasa wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambao matokeo yake yalikuwa ushindi kwa Rais wa zamani, Jakaya Kikwete, huku marehemu Lowassa akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Hata hivyo, marehemu Lowassa alidumu katika Uwaziri Mkuu kwa miaka mitatu hivi, ambapo mapema mwaka 2008 alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya umeme iliyohusu kampuni ya Marekani ya Richmond.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa marehemu Lowassa aliamua kujiuzulu ili kumnusuru rafiki yake (kwa wakati huo) Kikwete. Katika hilo, marehemu Lowassa alionyesha loyalty yake kwa rafiki yake, yaani Kikwete, ambaye aliendelea na urais hadi mwaka 2015.

Mwaka huo 2015, CCM haikupitisha jina la marehemu Lowassa aliyekuwa anawania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala, hali iliyosababisha ahamie Chadema ambako aliteuliwa kuwa mgombea urais kupitia umoja wa vyama vinne uliofahamika kama UKAWA.

Hata hivyo, licha ya marehemu Lowassa kuhamia Chadema, mmoja ya watu walioendelea kuwa marafiki zake wa dhati alikuwa Rostam, ambaye kwa wakati huo alikuwa amejiweka kando na siasa na kujikita kwenye biashara zake.

Kipimo cha loyalty ya Rostam kwa marehemu Lowassa kilikuwa baada ya uchaguzi huo ambao ulipelekea ushindi kwa marehemu John Magufuli ambaye alimwangusha marehemu Lowassa kwa tofauti ya kura chache.

Kwa bahati mbaya siasa za marehemu Magufuli zilitawaliwa na chuki za kisiasa na marehemu Lowassa alikuwa miongoni mwa wahanga wakubwa wa utawala huo. Kwa mujibu wa taarifa, kulikuwa na maagizo yasiyo rasmi kwa wana-CCM “wenye majina makubwa” walikuwa madarakani na nje ya madaraka kuhakikisha wanajiweka kando na Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Rostam alikabiliwa na uchaguzi mgumu: ahatarishe biashara zake kwa kuendelea kuwa loyal kwa marehemu Lowassa au amtenge ili asije kukumbana na “hasira za marehemu Magufuli”.

Lakini kama alivyofanya marehemu Lowassa mwaka 2008 ambapo alikuwa radhi kujiuzulu Uwaziri Mkuu ili kumnusuru rafiki yake Kikwete, ndivyo Rostam nae alivyoamua “liwalo na liwe” na akasimama bega kwa bega na marehemu Lowassa.

Ingeweza kuwa rahisi tu kwa Rostam kuamua kumtosa marehemu Lowassa ili anusuru biashara zake hasa kwa vile serikali ya marehemu ilikuwa ikimwandama mfanyabiashara huyo, lakini wanaomfahamu mfanyabiashara huyo wanasema kuwa “akishikamana nawe basi atasimama nawe hadi mwisho”.

Rostam na marehemu Mzee Cornel Apson

Marehemu Mzee Cornel Apson aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, alikuwa miongoni mwa watu wa karibu wa marehemu Lowassa kuelekea kwenye safari yake ya kuwania urais mwaka 2015 kupitia muungano wa vyama vya upinzani wa UKAWA.

Kitendo hicho kilipelekea mkuu huyo wa zamani wa ushushushu kuwa miongoni mwa wahanga wa “siasa za chuki za marehemu Magufuli”.

Kwa bahati mbaya, afya ya marehemu Apson ilidhoofika baadaye lakini kama ambavyo “watu mbalimbali hawakupaswa kuwa karibu na marehemu Lowassa ili wasije kukumbana na hasira za marehemu Magufuli”, ndivyo ilivyotokea kwa marehemu Mzee Apson pia.

Hata hivyo, mmoja wa watu wachache waliosimama bega kwa bega na marehemu Mzee Apson hususan wakati alipokuwa mgonjwa ni Rostam. Taarifa zinaeleza kuwa Rostam ndiye alikodi ndege iliyomsafirisha marehemu Mzee Apson kwenda matibabu nchini Afrika Kusini na pia ndiye aliyelipia gharama za matibabu hadi mauti yalipomkumba mtumishi huyo wa zamani wa serikali.

“Rostam alisimama nasi kama mwanafamilia hadi Mzee alipofariki, na alikuwa nasi kipindi chote cha msiba”, alieleza mwanafamilia mmoja.

Kadhalika, kabla ya marehemu Mzee Apson kuugua, Rostam aliweza kusuluhisha tofauti kati ya marehemu Magufuli na shushushu huyo mkuu wa zamani.

Rostam na mwalimu wake wa shule ya msingi

“Kwa utajiri wake mkubwa, unaweza kuamini kuwa rafiki yake mkubwa kabisa ni mzee mmoja huko Igunga ambaye alikuwa mwalimu wake wa shule ya msingi?” anaeleza mtu mmoja anayemfahamu vema mfanyabiashara huyo.

Mtu huyo alieleza kuwa mfanyabiashara huyo ni mtu loyal sana na hakushangazwa kuona ukaribu wake na marehemu Lowassa hata kipindi ambacho angetarajiwa kujiweka mbali na Waziri Mkuu huyo wa zamani kutokana na siasa za chuki zilizotawala zama hizo.

Rostam alivyowapatanisha Magufuli na Lowassa

Katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zilizokuwa zinaikabili serikali yake, marehemu Magufuli alilazimika kuwa na ukaribu na Rostam, hasa kwa minajili ya kuchuma uzoefu mkubwa wa mfanyabiashara huyo katika biashara za kimataifa sambamba na kuzielewa vema siasa za CCM.

Na mfanyabiashara huyo hakuchukua muda mrefu kutumia nafasi hiyo kumpatanisha marehemu Magufuli na hasimu wake wa kisiasa marehemu Lowassa, ambaye hatimaye alirejea CCM.

Hitimisho:

Katika zama hizi za watu kuombeana mabaya kama sio kushiriki kwenye hujuma hata dhidi ya marafiki zao, kuona kwamba bado kuna watu wanaothamini loyalty kama Rostam ni jambo linalopaswa sio tu kupongezwa bali pia kuenziwa.

Miongoni mwa nukuu maarufu sana kuhusu loyalty ni hii pichani inayomaanisha kwamba damu huwafanya mtu kuwa ndugu, loyalty humfanya mtu kuwa familia

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles