28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa ni pasua kichwa (2)

Edward Lowassa
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa

Na Absalom Kibanda,
TAIFA linazidi kujongea kuelekea katika kilele cha kelele za shangwe na majonzi yatakayotokana na uteuzi wa wagombea na baadaye matokeo ya ama kushinda au kushindwa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa maneno mengine, hali hiyo inaeleza kuwadia kwa msimu wa Uchaguzi Mkuu ambao kwa utamaduni wa miaka ya hivi karibuni hutawaliwa na kila aina ya vituko vinavyohusisha na kugusa watu wazito.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, uzito wa watu hao umenilazimisha hata mimi kwa wiki ya pili sasa kujikuta nikishindwa kuiepuka dhambi ya lazima ya kujadili majina ya watu badala ya kujadili masuala ya msingi ambayo yangepaswa kuwa ajenda za kutuandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwamba anaibuka Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya na kumsuta mtu anayeishia kumsema pasipo kumtaja jina na kisha kueleza wasifu wa ‘mbaya wake’ huyo kwa namna ya kuonyesha alivyo na tope mwilini si jambo la kulipuuza na kuliacha likapita.
Kama nilivyobainisha wiki iliyopita, utakuwa ni uamuzi wa hovyo iwapo nitaacha pasipo kuichambua kauli nzito ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mzee wetu Philip Mangula aliyeeleza kupata taarifa za kuwapo kwa kada mmoja wa chama hicho mwenye mipango ya urais anayetuhumiwa kutoa rushwa Zanzibar.
Kauli hiyo ya Mangula ambayo katika kipindi cha siku mbili mfululizo baada ya Krismasi ilinukuliwa katika magazeti matatu, likiwamo gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), si ndogo au nyepesi ya kuachwa ikapita pasipo kunyumbulishwa.
Mwangwi wa matamshi ya namna hiyo ya Msuya na Mangula ulioonekana kuakisiwa pia na akina January Makamba na Bernard Membe ambao pia wao wenyewe kwa staili na namna tofauti wameeleza kusudio lao la kuutaka urais, unapaswa pia kuchambuliwa ili kuwapa fursa Watanzania kupembua, pumba na mchele.
Mambo kadhaa yametokea katika kipindi cha siku sita zilizopita na kuthibitisha kwamba kile nilichokiona wiki iliyopita na kuchukua muda wa kukichambua hakikuwa kitu kidogo cha kupuuzwa kwani mvumo wa upepo wake umeendelea kusikika.
Uamuzi wa vigogo na wakongwe wa siasa wa aina ya Kingunge Ngombale – Mwiru na Pancras Ndejembi kujitokeza na kutoa kauli zao kuelezea mustakabali wa taifa na maandalizi ya kugombea urais baadaye mwaka huu ni ushahidi mwingine kwamba kile nilichoanza nacho Alhamisi iliyopita kilikuwa ni hoja sahihi iliyokuja kwa wakati wake.
Hoja kadha wa kadha zimeibuliwa na kubwa katika hizo ni ile ya matumizi makubwa ya fedha katika kusaka nafasi ya uteuzi wa nafasi ya kugombea kwa tiketi ya CCM, chama ambacho kama halitatokea jambo kubwa na zito la kukipasua vipande viwili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, basi kinapewa nafasi kubwa ya kuendelea kuongoza taifa kwa miaka mingine mitano.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, hofu inayoonekana kuwagusa baadhi ya watu walioonyesha nia ya kutaka kugombea urais mwaka huu haipo katika kiu ya kusaka majibu ya maswali magumu yanayolikabili taifa hili bali katika ushindani wa wao kwa wao.
Ukisikiliza kauli za takriban wagombea wote walioanza kutoa kauli za kusaka urais au kuonyesha nia hiyo, jibu unalopata haraka haraka ni ubinafsi uliovuka mipaka, kujikweza kusikokoma, kutishana na kufitiniana wao kwa wao.
Kwa bahati mbaya, historia ya madhambi ambayo wana CCM waliyafanya wakati taifa likielekea kumpata mgombea urais mwaka 2005 inaonekana kujirudia na kutunyemelea tena kwa bashasha zile zile japo walengwa wa sasa si wale tena na mazingira ya leo ni tofauti kidogo na yale yaliyopita.
Nililisema hili wiki iliyopita na leo nalisema tena kwamba, katikati ya fitina zote hizi ambazo aghalab zinajaribu kuficha majina ya watu, mlengwa nambari moja ni mmoja wa wanasiasa ambaye anatajwa kuwa kinara wa mbio za urais mwaka huu.
Mwanasiasa huyo si mwingine bali ni Edward Lowassa, mtu ambaye jina lake linatajwa sana kwa mafumbo na kwa uwazi na kugusa kwa wema au kwa ubaya viunga vya fikra za viongozi na makada wenzake wa CCM, maadui na marafiki zake.
Ndani na nje ya CCM, kwa muda wa miaka 20 sasa jina la mwanasiasa huyo limetawala mijadala ya kisiasa na kiuongozi kwa namna (si kiwango) ambayo hadi sasa tafakuri yangu haijapata kumfananisha na mwingine yeyote wa kariba au kizazi chake.
Taswira na haiba yake ya kisiasa na kiuongozi imemjengea marafiki lukuki na maadui wengi ukiachilia mbali wafuasi na mashabiki wa kutosha sawia pia wapinzani wake wakubwa.
Leo hii yanapoibuka makundi ya watu kumsifu au kumpamba, kumsuta, kumkashifu, kumtukana na hata kumpuuza, huwa sishangazwi hata kidogo na hali hiyo kwa kuwa, angalau utafiti mdogo nilioufanya kuhusu mwanasiasa huyo huwa unanipa majibu mengi tofauti.
Si ajabu hata kidogo, mwaka 2009, miezi kadhaa baada ya kujiuzulu kwake uwaziri mkuu kwa shinikizo la sakata la Richmond na kwa kutambua mazingira yaliyokuwa yakilizonga jina lake, niliandika makala yenye kichwa cha habari; “Taifa linaugua homa ya Lowassa” ambayo iliibua maswali, chokochoko na kelele nyingi sana.
Leo hii miaka mitano baada ya makala ile bado mtazamo wangu kuhusu jambo hilo ni ule ule na akitokea mtu akaniuliza naweza nikaielezaje hali hiyo, basi jibu langu ni rahisi kabisa; ‘homa imepanda na joto limekuwa kali zaidi.’
Huyo ndiye Edward Lowassa ambaye leo hii anasakamwa na akina Msuya, anachunguzwa na kina Mangula na kukosolewa na watu wa kariba ya Bernard Membe, Anthony Diallo na kabla yao Samuel Sitta na Dk Harrison Mwakyembe.
Mbali ya hao ni Lowassa huyo huyo ambaye ananyoshewa vidole na vijana wa aina ya January, Khamisi Kigwangallah, Nape Nnauye, Paul Makonda na wengine kadhaa.
Tofauti na hao, Lowassa anao wafuasi na watu wanaomuunga mkono na kumpigania wa aina ya Bakari Mwapachu, Kingunge Ngombale Mwiru, John Guninita, Sophia Simba, Hussein Bashe, Peter Serukamba na wanasiasa wengine kadhaa.
Hawa wote ni wachache tu kati ya wengi walio ndani ya CCM ambao haiba na taswira ya kisiasa ya Lowassa imewakoroga vilivyo kwa kiwango kile kile ambacho wanasiasa wengine kadhaa ndani na nje ya chama hicho wako.
Kwa ukaribu, Lowassa anaweza akalinganishwa kwa namna fulani ya kiushawishi na hasa zinapokuja hoja za kudhulumiwa na kusutwa kama si kwa kuonewa na alivyo jabali la siasa za kishindo Zanzibar, kioo cha fikra mbadala ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Wakati Lowassa akiwa gumzo la siasa za kitaifa kwa takriban miaka 20 na ushee sasa, Maalim Seif yeye amekuwa kinara wa siasa za ushindani akitajwa kwa mema na mabaya na kishindo chake kuitikisa vilivyo CCM kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Kwa sababu tu ya hulka ya kupenda siasa na kuguswa na masuala yanayouzonga uongozi wa taifa langu, nyakati na kwa njia tofauti, ushawishi mkubwa wa wanasiasa hao wote wawili ulinisukuma kupenya katika ngome zao na kuruka vihunzi vya kila namna kabla ya kuwafikia na kujua siri zilizokuwa nyuma ya kutajwa kwao sana kwa wema na kwa ubaya.
Katika kufanya hivyo, kama mwanahabari, mhariri na mchambuzi nimekutana na kuzungumza na wanasiasa hao wawili mara kadhaa, nikasoma taarifa zao nyingi, nikateta na marafiki na mahasimu wao kwa miaka mingi sasa.
Si hayo tu, naweza nikasema pasipo kumung’unya maneno kwamba, nimewafuatilia kwa karibu wanasiasa hao wote wawili kwa kiwango cha kuzigusa hata familia zao, ndugu na jamaa zao na kwa namna na njia tofauti nikafanya nao kazi zilizonipa fursa ya kujua kile ambacho katika hali na mazingira ya kawaida nisingeweza kukipata au kukifahamu.
Nikianzia na Lowassa, pengine katika hili ni busara nikawashirikisha Watanzania wenzangu kwa kueleza kwamba, nilifanya yote haya nikitimiza wajibu wangu na kutafuta ukweli wa ndani ambao kwa njia za kawaida nisingeweza kuupata.
Nilianza kufuatilia nyendo zake za kisiasa na kiuongozi kwa ukaribu mkubwa tangu ushawishi wake ndani ya Bunge wakati akiwa Waziri wa Ardhi na Nyumba kwenye serikali ya Awamu ya Pili, miaka ya mwanzo ya 1990 alipowahamasisha vijana wa Dar es Salaam kuvamia na kubomoa uzio wa mabati uliokuwa umejengwa kuzunguka viwanja vya kihistoria ya Mnazimmoja.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wangu wa kumfahamu kwa njia ya kumsikia, mwanasiasa huyo ambaye siku nisiyoikumbuka alisimama ndani ya Bunge na akazungumza kwa kujiamini, akieleza masikitiko yake kuhusu kuvamiwa kwa viwanja vya kihistoria vya Mnazimmoja na tajiri aliyedaiwa kuuziwa eneo hilo na viongozi wa Jiji la Dar es Salaam.
Ingawa zama hizo, vikao vya Bunge vilikuwa vikirushwa na Radio ya Taifa peke yake, kabla ya teknolojia ya televisheni kusambaa, uchungu uliobeba hisia za Lowassa kueleza hisia zake kuhusu ufisadi huo, ziliibua makundi ya vijana waliovamia eneo zima la Mnazimmoja na kung’oa na kuondoka na mabati yote yaliyojenga uzio wa eneo hilo.
Nikiwa kijana mdogo na mdadisi sana nyakati hizo, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilijikuta nikiguswa na Lowassa na mara moja katika misingi ya kiudadisi nilijikuta nikifuatilia kwa karibu kwa namna ile ile ilivyokuwa desturi ya vijana wengi wa zama zile.
Miaka hiyo, halikuwa jambo la ajabu hata kidogo kwa vijana wa sekondari na vyuo kushiriki katika mijadala ya wazi na ile ya kupangwa iliyokuwa ikijadili kauli, matendo na maamuzi mbalimbali ya viongozi wa kiserikali, kisiasa, kijamii na hata kidini.
Kwamba nyakati hizo hizo nilikuwa tayari nimeanza kuandika makala za siasa na uongozi katika magazeti mbalimbali, nilipaswa kujipanga sawa sawa kifikra na kukuna bongo yangu vizuri kabla ya kuwashawishi wahariri mahiri wa zama hizo kuyakubali maandiko yangu.
Halikuwa jambo rahisi kuwashawishi wahariri wa kariba ya Jenerali Ulimwengu, John Rutaysingwa, Salvatory Rweyemamu, Henry Kilimwiko, Kajubi Mukajanga, Ben Mtobwa na wengine wengi wa zama hizo ili wachape makala ya kichambuzi katika magazeti ambayo yalitawaliwa na nguvu ya hoja.
Ili kuweza kuwekwa katika daraja la wachambuzi- watafiti, moja ya mambo ambayo niliyafanya kwa kulazimika lilikuwa ni hilo la kupekuapekua undani wa kila kinachoandikwa na kusemwa kwa kiwango cha kuyaelewa mambo mengi kwa kina na kwa mapana.
Ni katika misingi hiyo hiyo ya kihabari na kichambuzi, nilimfuatilia Lowassa kwa karibu na chachu ya kudadisi ukweli mwingi juu yake kama nilivyofanya kwa wengi wengine iliongezeka wakati yeye na rafiki yake kikazi, Jakaya Kikwete (sasa Rais wa Tanzania) walipotangaza kwa pamoja uamuzi wa kugombea urais wa Tanzania mwaka 1995.
Kishindo cha uamuzi wa Lowassa na Kikwete kugombea nafasi hiyo kilinisukuma kuwafuatilia kwa karibu kabla ya ushawishi kuongezeka baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuweka mguu kati na kumzuia mmoja wao.
Kwa bahati njema au mbaya, aliyekumbana na kikwazo cha Nyerere alikuwa ni Lowassa ambaye aliingia katika mchuano wa urais kwa kishindo kikubwa na kutikisa vilivyo vikao vya taifa vya uteuzi ndani ya CCM.
Aliporejea Dar es Salaam baada ya jina la Lowassa kuondolewa katika mchujo, kwa maneno yake mwenyewe, Nyerere aliwaeleza waandishi wa habari pamoja na mambo mengine kwamba ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC); “Jina la Lowassa lilijadiliwa kwa ushabiki mkubwa.”
Taswira hiyo juu na dhidi ya Lowassa ndiyo ambayo imeendelea kubakia kuwa baraka na laana kwa marafiki na maadui wa mwanasiasa huyo ndani na nje ya CCM ambao wamekuwa wakiongezeka idadi kila siku iitwayo leo.
Si ajabu hata kidogo kwamba, mahasimu wake ndani ya CCM wakiwamo wale wanaojitokeza leo kumsuta na kumshambulia kila wakati na hasa tangu akiwa Waziri Mkuu na baada ya kulazimika kujiuzulu wanaujua ukweli huo wa kihistoria ambao yumkini mwanasiasa huyo anaonekana kuutumia kujipanga na kupanda ngazi.
Ushawishi alioujenga kwa miaka nenda, miaka rudi umeendelea kumuongezea marafiki na maadui na sasa baadhi ya wale ambao taswira na haiba yake imekanyaga nyayo zao wanatoka wakimlaani kwa gharama ambazo huko TUENDAKO si tu kwamba zitabebwa na yeye binafsi, bali pia chama tawala na pengine taifa zima.
Tutaendelea na mada hii wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles