*Lowassa asema anatosha kupambana na umaskini
*Sumaye ataka CCM waanze kuondoa hirizi Ikulu kama wameziacha
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema yeye ndiye anayetosha kupambana na umaskini wa wananchi huku Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, akiitaka CCM ianze kuondoa hirizi Ikulu kama zipo kwa vile Ukawa wanaingia madarakani.
Waliyasema hayo kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika wilayani Temeke Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Tungi Kigamboni, Lowassa alisisitiza lengo lake ni kupambana na umaskini.
“Nitaanza na elimu kutoka shule ya watoto wadogo hadi elimu ya juu ambayo itakuwa ni bure… elimu ni muhimu kuanzia kwa mtoto mdogo hadi elimu ya juu.
“Baada ya elimu kinachofuata ni kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya mama lishe, wamachinga na bodaboda , kufungua viwanda kwa ajili ya ajira kwa vijana.
“Mkinichagua baada ya kuapishwa nitaanza na kivuko cha feri ambako wananchi mtavuka bure bila malipo yoyote,” alisema Lowassa.
Akiwa kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya Chanika Magengeni wilayani Temeke, alisema anawashangaa baadhi ya watu wanaofuatilia safari zake zikiwamo ziara zake sokoni na kwingineko wakati wanaosafirisha wanyama hai nje ya nchi wakiwamo twiga, hawahojiwi.
Alisema hata alipopanda daladala baadhi ya watu walihoji kitendo hicho lakini bado wamekuwa hawahoji waliopeleka twiga nje ya nchi.
Lowassa alisema kwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wamechoka kula mlo mmoja na kwamba wanahitaji maisha mazuri ambayo watayapata kwa kufanya mabadiliko.
“Wananchi wanahitaji mabadiliko na maisha mazuri, nina imani fedha za kufanya haya yote zipo …tutatoa elimu bure kuanzia shule za watoto wadogo hadi Chuo Kikuu kwa kuwa uwezo huo upo, kama fedha hamna mbona mashangingi kila siku yanaongezwa?” alisema Lowassa.
Sumaye
Naye Sumaye alisema ni vema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiandae kuachia Ikulu na kama kuna kirizi kilizoweka kizitoe kwa sababu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaingia madarakani.
“Kama kuna hirizi ama kitu kingine ambacho wamekisahau, sasa muda umefika watoe kila kilicho chao kwa sababu Ukawa wanaingia madarakani,” alisema Sumaye.
Alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ni sawa na mtu aliye kwenye kitanda ambacho kina wadudu ikizingatiwa chama chake kilivyo hivyo kumchagua ni kuendelea kupoteza mwelekeo wa maendeleo.
“Kitanda chenye wadudu kinachomwa moto, hivyo Magufuli anafananishwa na kitanda hicho …kama vipi aje Ukawa akishindwa tutamtupa porini na kitanda chake,”alisema Sumaye.
Sumaye alisema nchi ipo katika kipindi ambacho wananchi wenyewe wana hiari ya kuamua kujikomboa au kubaki katika shida huku wana CCM wakiendelee kushiba.
Alisema ana imani wananchi wanahitaji mabadiliko lakini kwa kuichagua CCM hakuna matumaini mbele yao.
“CCM lazima iondoke madarakani, haiwezi kuangalia afya ya wananchi … ni aibu mno eti Dar es Salaam tunaugua kipindupindu ni aibu sana,”alisema Sumaye.
Alisema anamshangaa Magufuli kudai eti nchi ni yake wakati hajapata ushindi na kuhoji endapo atapata ushindi wao wataishi wapi.
“Namshangaa Magufuli kusema nchi yake, je akishinda sisi wengine tutajificha wapi?” alihoji Sumaye.
Alisema pia kwamba CCM inatoa maneno ya vitisho kwa wananchi lakini wao Ukawa hawasumbuki bali watafanya siasa ya amani na demoktasia.
Alisema watakaosababisha machafuko ni CCM kwa kukataa demokrnasia ya wanachi kwa sababu Ukawa wanahitaji amani.
Mgombea ubunge wa Kigamboni, Lucy Mageleli alisema Lowassa ni kama Musa aliyekuja kuwakomboa watu wa Kigamboni kutoka utumwa wa CCM.
Alisema Serikali ya Lowassa ikiingia madarakani itahakikisha umaskini kwa watu wa Kigamboni unaisha na Mungu atawapa nchi yenye asali na maziwa.
“Wananchi kivuko siyo starehe ni sehemu yetu na ni haki yetu hatutakiwi kukilipia, pia hayo magari ya Ridhiwani yanayoegeshwa hapo kusubiri wamanchi tutakapoingia madarakani yataondoka na tutabakia na daladala zetu za Buguruni, Mbagala na Gongo la mboto.
Duni
Naye mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma haji Duni, alisema taifa linahitaji mabadiliko ya fikra kwa kupata elimu bora, nafasi mpya ya kufikiri akisema CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake.
Alisema mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anataka urais aliahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania lakini hali hivi sasa imekuwa mbaya zaidi ya awali.
“Hata huyo Magufuli kwanza hatufai kwa kuwa yeye kila kitu anashangaa tu kama ilivyo kwa mwenzake ambaye alikuwa anacheka twiga wanaondoka, yeye anacheka… kila kitu yeye anacheka tu.
“Tunahitaji mabadiliko tena ya fikra … inatupasa kupata elimu hivyo ni lazima kila mtu apate haki hiyo na Lowassa si mtu wa kuchekacheka,” alisema.
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wananchi wamekubaliana kuwa mwaka 2015 wamechoka maumivu na wanachohitaji ni mabadiliko tu.
“Wananchi wamechoka, wanahitaji mabadiliko na ndiyo maana hata sisi tumesimamisha mgombea mmoja tu wa Ukawa,”alisema Mbowe.
Akifafanua kuhusu mkanganyiko wa mgawanyo kwa wagombea katika kuwania udiwani na ubunge katika Ukawa, alisema kauli ya wengi ni ya Mungu, kwa pamoja walikaa na kuamua kumsimamisha mgombea mmoja kutoka chama chochote anayekubalika katika kila kata na jimbo.
Mbowe alisema ili waende na kasi ya mabadiliko ni lazima wapate mgombea makini na anayekubalika kwa umakini wake.
“Natoa saa 48 kwa viongozi mbalimbali kufanya uamuzi wa kuwapitia wagombea ambao wana sifa… awe wa chama chochote ili mradi wa ushirika wetu na atakayekiuka haya tutamfukuza, hatuna haja ya kubembelezana,”alisema Mbowe.
Hata hivyo, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuona umuhimu wa kushughulikia kauli iliyotolewa na kiongozi mmoja wa CCM aliyedai CCM kitaachia majimbo yote na kata lakini si Ikulu.
MABANGO
Wananchi hao muda wote walikuwa wakishangilia huku waionyesha mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali.
Baadhi yaliandikwa, ‘Toroka uje Ukawa ndiyo mpango mzima’, ‘Malofa katika ubora wetu’, ‘Vijana Chanika tulitumika na CCM sasa zamu ya Ukawa’, ‘Tumeikataa CCM jumla tunataka mabadiliko’, ‘Wazee wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tusaidiwe’.
Mengine yalisomeka, ‘Magufuli huwezi kuitengeneza injini ya gari ukiwa ndani ya gari bovu shuka uichungulie injini hiyo…hamia ukawa’.
Mengine yalisema, ‘Tunamchagua Lowassa kutoka UKAWA maendeleo yatakuja’, ‘mchawi mpe mwana akulelee’, ‘heri Kipindupindu kuliko CCM’, ‘miaka 50 ya kudanganywa inatosha’, ‘M4C bado tuna imani na Lowassa hatuyajali maneno mnayoyasema wembe ni ule ule’ na wengine walikuwa na msalaba uliokuwa umeandikwa ‘John Pombe Magufuli kuzaliwa mwaka 1961 kifo 25, Oktoba 2015’.
Habari imeandikwa na CHRISTINA GAULUHANGA,
ADAM MKWEPU NA ASIFIWE GEORGE, Dar es Salaam