23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sumaye: CCM haishindi

IMG_5192*Asema mizani haijalalia upande mmoja, aponda utafiti wa Makamba

 

HERIETH FAUSTINE NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema endapo haki itatendeka kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitashinda kwa sababu mwaka huu mizani haijalalia upande mmoja kama ilivyozoeleka.

Sumaye aliyasema hayo jana wakati akihojiwa moja kwa moja katika kipindi cha Funguka na Kituo cha Televisheni cha Azam, jijini Dar es Salaam.

Alisema endapo kanuni na sheria za uchaguzi zitafuatwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utakuwa na nafasi nzuri ya kupata ushindi kwenye  uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Alisema kwa hali ilivyo hivi sasa ni dhahiri kwamba CCM itafanya vibaya kwenye ngazi za udiwani, ubunge na urais.

“Sisi kama Ukawa hatutafanya tathmini  ya aina yoyote ila tunachoangalia hali ilivyo na mwamko wa wananchi  unaonyesha hakuna sehemu ambayo CCM itashinda.

“Kwa jinsi mambo yalivyo na iwapo uchaguzi utafanyika huru na haki sioni kwa namna gani Ukawa isishinde uchaguzi mkuu. Kama ni haki bini haki CCM haishindi,” alisema Sumaye.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, hakuna anayemdharau mwingine kutokana na ushindani uliopo hivyo Watanzania watapata manufaa ya demokrasia ya vyama vingi.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi nchini, upinzani umekuwa mkubwa, CCM itapata changamoto kubwa katika ngazi zote na wananchi watapata demokrasia ya kweli,” alisema Sumaye.

Alisema kama upinzani utashinda na kuamua kuchukua watu kutoka vyama tofauti tofauti kwa ajili ya kuunda Serikali, litakuwa ni jambo zuri kwani hata Katiba inaruhusu kufanya hivyo.

 

Tathmini iliyofanywa na CCM na kutolewa na Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, January Makamba, kwamba itashinda kwa asilimia 69, Sumaye alisema hiyo ni propaganda za kisiasa na zilizochochewa na taarifa za kwenye mitandao ya kijamii zilizodai chama hicho tawala kina hali mbaya.

Alisema CCM inafanya mambo mengi ili ishinde ikiwa ni pamoja na kutuma vijana maeneo mbalimbali nchini ili waandike namba za shahada za wapiga kura jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Kazi hii ingefanywa na Ukawa hao vijana wangekamatwa na kuwekwa ndani… zile kadi si mali ya CCM wala Serikali ni mali ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Ukawa wangefanya haya wangekuwa wamekamatwa na kuwekwa ndani, tuache demokrasia ichukue mkondo wake,” alisema Sumaye.

HATIMA YAKE

Kuhusu hatima yake kisiasa, alisema endapo hata Ukawa wasipofanikiwa kushinda uchaguzi mkuu atabaki upinzani ili kuimarisha demokrasia ya kweli.

“Ikitokea Ukawa tukashindwa uchaguzi wa mwaka huu, nitabaki upinzani na nitajiunga na chama chochote ili kuendeleza na kuimarisha demokrasia ya kweli,” alisema Sumaye.

Alisema CCM iligundua upinzani hauna nguvu ndiyo maana walikuwa wanalala katika kufanya kazi zao sasa yeye kuhamia upande wa pili ndiyo siasa yenyewe kwani hawatalala tena.

“CCM miaka ya nyuma haikuwa na upinzani mkali ndiyo maana walikuwa wanafanya mambo halafu wanalala, lakini sasa wameanza kuona tofauti yake,” alisema Sumaye.

MAJIMBO

Akizungumzia kuhusu mvutano wa majimbo na viongozi kutoshiriki katika kampeni, Sumaye alisema muungano wa vyama hivyo una mambo mengi hivyo katika hali hiyo yapo mengi yatakayotokea.

RICHMOND

Alipoulizwa kuhusu kashfa ya Richmond, Sumaye alisema: “Ningekuwa rais ningemtaja mhusika wake…unaponiuliza hapa simjui, yule aliyewataja ndiye anapaswa kumtaja.

“Alitaja kumi akiwako Kikwete (Rais)  na Mkapa (Rais mstaafu Benjamin), huyo ndiye anayepaswa kumtaja tena kwani hao 10 wako upinzani? “Namjua Mkapa si fisadi… sifanyi siasa za kubahatisha na kamwe siwezi kuwa kasuku wa kutaja majina ya watu.

Alipoulizwa kuhusu kutozungumzia suala la ufisadi baada ya kutoka  CCM, Sumaye alisema amekuwa akilisema kila anapopata nafasi ya kuwa jukwaani na kusisitiza kuwa ataendelea kukemea rushwa.

Akijibu swali la mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, kutoitangaza ilani ya chama katika majukwaa, alisema kampeni sio darasa linalotaka uorodheshe kila kitu ubaoni bali unaangalia vitu muhimu na vingine unavieleza ukipata nafasi.

“Kuna vitu vya muhimu katika ilani yetu kama elimu, viwanda, ajira na kilimo, hivi ni lazima uvieleze mara kwa mara kutokana na umuhimu na ndiyo maana huwa anavirudia kuvitaja,” alisema.

Kuhusu gharama za elimu, alisema  wameandaa mkakati katika matumizi ya fedha na ukasanyaji wa kodi endapo  zikitumiwa ipasavyo elimu inaweza kutolewa bure.

“Elimu bure si gharama za ajabu, tatizo matumizi yasiyo na mpangilio, mabadiliko makubwa lazima yaanzie kwenye sera,” alisema Sumaye.

Akijibu swali kuhusu kushindwa kuleta mabadiliko katika kipindi cha miaka 10 aliyokuwa waziri mkuu, alisema mabadiliko ni lazima yaanze na sera na katika kipindi hicho waliweza kutoa elimu ya msingi bure na kupunguza gharama za elimu ya sekondari.

“Kipindi naingia madarakani nilikuta shule nyingi wanafunzi wanakaa chini, ndani ya mwaka mmoja niliweza kufanikiwa shule zote kuwa na madawati na hii ilitokana na kufanyiwa kazi sera,” alisema Sumaye.

Alisema alivyokuwa akiingia madarakani hali ilikuwa mbaya katika huduma za jamii kama maji, hospitali kutokuwa na dawa, lakini alifanikiwa kutoa huduma hizo.

Alisema anapatwa na uchungu anapoona yale yote aliyoyafanya katika uongozi wake kutokuwapo sasa ambapo shule nyingi nchini wanafunzi wanaendelea kukaa chini huku maendeleo ya sekta nyingine yakizidi kudidimia.

“Katika awamu ya tatu tulifanya kazi kubwa, mimi binafsi nilikuwa nashindwa kwenda likizo wakati mwingine nalazimika kuahirisha safari za nje ya nchi, leo tumerudi nyuma katika huduma za jamii, ukweli nasikia uchungu wanafunzi wanapokaa chini,” alisema Sumaye.

MASHAMBA

Kuhusu mashamba yake, Sumaye alikiri kumiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 300 katika eneo la Mvomero na si Kibaigwa kama inavyodaiwa.

Alisema eneo hilo liliuzwa kutokana na kuwa na madeni ya benki.

Alisema alifuata taratibu zote kununua shamba hilo na hajawahi kuwa na shamba eneo la Kibaigwa kama inavyodaiwa na washindani wake wa kisiasa.

“Sisi tunaishi katika ulimwengu huu na hukuna kinachojificha, mimi sina biashara zaidi ya shamba lililopo Mvomero, hili shamba liliuzwa na kutangazwa kwenye magazeti na sijawahi kuchukua shamba la magereza hata akiulizwa Mkuu wa Magereza,” alisema.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles