27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa gumzo tena bungeni

Edward Lowassa
Edward Lowassa

Na BAKARI KIMWANGA-DODOMA

JINA la aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, limetikisa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kuanza kuimba wimbo kwa kutumia jina lake.

Tukio hilo lilitokea jana mjini hapa wakati wa mjadala Muswada wa Sheria za Huduma ya Vyombo vya Habari wa mwaka 2016, baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM), kulitaja jina la mgombea huyo kuwa alisafishwa na vyombo vya habari ambapo vilidai kuwa alikuwa ni fisadi.

Amina ambaye kitaaluma ni mwanahabari ambapo alikuwa akinukuu vichwa vya habari zilizowahi kuchapishwa kwenye gazeti la Mwanahalisi, alimtaja Lowassa kama ni moja ya mtu mwenye kasoro kiuongozi huku chapisho lingine likimsifu kwa kumkaribisha kujiunga na Chadema.

“Mheshimiwa mwenyekiti, uandishi wa aina hii ambao leo unamwandika mtu kwa kumwelezea kuwa hafai na baadaye unamsafisha na kumkweza, haina budi utungiwe sheria itakayowadhibiti,” alisema Amina.

Kutokana na hoja hiyo ambayo ilijibiwa kwa semi na mafumbo na Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), alimtaka Amina kuwa mtu wa mwisho kuwakejeli watu wanaompenda Lowassa.

“Waswahili husema unapokwenda kwa wenye chongo fumba lako jicho ili unene nao. Ni ajabu sana hapa leo hii imekuwa ni vijembe na kejeli kila kukicha hasa kwetu sisi tunaompenda Lowassa.

“Ninamshangaa mzungumzaji aliyepita ambaye kila wakati amekuwa akilitumia jina la Lowassa kujenga hoja zake. Haya si mageni, sheria mnatunga nyie CCM na si mlikuwa mkiimba kila siku Lowassa fisadi kwanini msimfikishe kwenye vyombo vya sheria.”

Khatibu alisema mnaponyoosha vidole vyenu (wabunge wa CCM) kwa wanaompenda Lowassa, hamweleweki hata kidogo, labda niwakumbushe kidogo; “Kweeeliiii…,”

Kibwagizo hicho kilipokewa na wabunge wengine walioendeleza kwa kuimba, “Kweli, kweli, kweli Lowasaa..” kabla ya Mwenyekiti wa kikao, Andrew Chenge, kuingilia kwa kuzuia aina hiyo ya uchangiaji.

Awali, baada ya mchakato wa kupata mwakilishi wa CCM katika kugombea urais wa Tanzania, Lowassa alikuwa miongoni mwa watu 40 waliotia nia ya kugombea nafasi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisimama na kuwataka wabunge kuacha kutaja jina la mtu ambaye hayupo bungeni kwani hana haki ya kujitetea kwa wakati huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles