Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Arusha, Fredrick Lowassa, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada na kuhakikisha chanjo ya ugonjwa wa Corona inapatikana haraka akianza kusambaza dozi 1,050,000 nchi nzima.
Lowassa amesema yeye amekuwa mtu wa 972 kupata chanjo ya Covid 19 katika Wilaya ya Monduli iliyozinduliwa wilayani humo na Mkuu wa Wilaya, Frank Mwaisumbe, Agosti 3, 2021.
Amesema kuna watu wachache wanajaribu kubeza, lakini wakumbuke hii siyo kazi rahisi hata kidogo,ukizingatia msimamo wa nchi yetu ulivyokuwa dhidi ya janga hili hapo nyuma.
“Dunia nzima imeamini kwamba njia sahihi na ya kisayansi ya kujikinga na janga hili la Corona ni hizi chanjo zilizothibitishwa na WHO (World Health Organisation).
“Ndugu na marafiki zetu wengi wanafariki kila siku kwa janga hili la Covid-19, unadhubutu vipi kumshawishi mtu asichanje wakati haujampatia mbadala wowote wa kujikinga?
“Kipekee, nimshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa sana, hasa tukizingatia kwamba amekuwa Rais ndani ya muda mchache sana”, amesema Lowassa.
Pia amewapongeza wahudumu wa afya wa Monduli na nchi nzima kutokana na kuhangaika kila siku kuhatarisha maisha yao ili kuokoa ya wengi.
“Naomba Wanamonduli na Watanzania wenzangu tuwapuuze, tukajilinde dhidi ya Janga hili, lakini zaidi tuendelee kumuunga mkono na kumtia moyo Rais,” ameeleza.