Na JONAS MUSHI – DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amesema Cuba ni taifa dogo lililoitikisa dunia kwa sababu ya uongozi imara wa aliyekuwa Rais na mwanamapinduzi wa nchi hiyo, Fidel Castro.
Lowassa ambaye pia ni na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliyasema hayo jana Dar es Salaam, nyumbani kwa Balozi wa Cuba nchini, Jorge Luis Lopez Tormo, alipofika kumpa pole na kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Castro kilichotokea Novemba 25, mwaka huu jijini Havana Cuba.
Alisema kiongozi huyo ni mwanamapinduzi aliyemhamasisha kwa namna alivyokuwa akifanya kazi ya kuwatetea wanyonge na masikini kote duniani.
“Castro alikuwa mtu mwenye maono na misimamo ya kile alichokiamini na kuifanya Cuba pamoja na udogo wake itikise dunia, ukienda kila mahali unamsikia Castro… ni mwanamapinduzi aliyefanya kazi ya kuwatetea wanyonge na masikini na dunia ilimfahamu hivyo. Alini-‘inspire’ (hamasisha) kwa sababu alikuwa ‘focused’ na mwenye kusimamia kile alichokiamini,” alisema Lowassa.
Castro alikuwa mwanamapinduzi wa miaka ya 1950 ambaye alimpindua aliyekuwa kibaraka wa Marekani, Rais Fulgencio Batista mwaka 1959, baada ya kuendesha vuguvugu la watu waliokuwa tayari kuipinga Serikali iliyokuwa imetawaliwa na rushwa na anasa zilizofanywa na wawekezaji kutoka Marekani.