25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa alalamika kuchezewa rafu na polisi

Pg 2 oktb 27SHABANI MATUTU NA MAULI MUYENJWA

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amelalamikia rafu alizodai kuchezewa na Jeshi la Polisi kwa nia ya kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Malalamiko hayo ameyatoa jana, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Lowassa, Jeshi la Polisi limewakamata vijana 192 wa chama hicho waliokuwa wakifanya kazi ya kupokea na kujumlisha matokeo ya nchi nzima.

Baada ya vijana hao kukamatwa juzi katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema walibambikiwa kesi ya usafirishaji wa binadamu.

“Jeshi la Polisi limewakamata vijana wetu waliokuwa wakifanya kazi ya upokeaji wa matokeo na kuwabambikia kosa kubwa la ‘human trafficking’.

“Kazi iliyokuwa ikifanywa na vijana hao si kosa kisheria kwa sababu wao walikuwa na nia ya kufuatilia historia ya uchaguzi wa nchi yao.

“Nimesikitishwa na utendaji wa Jeshi la Polisi kwa kuwavamia vijana hao katika maeneo yao ya kufanyia kazi katika Hoteli ya Misuma, Mwananyamala muda wa saa sita usiku na kuwakamata vijana 26.

“Vijana wengine walikamatwa eneo la Hoteli ya Nemax, Kinondoni majira ya saa tisa alfajiri jana.

“Baada ya kupata taarifa hiyo, nilimpigia simu Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu na kumwelezea  tatizo hilo na aliniahidi kulifanyia kazi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika,” alisema.

Alisema pia kwamba baada ya vijana hao kukamatwa, walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na wameshikiliwa hadi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Katika ufuatiliaji wa suala hilo, alisema Chadema waliandika barua kwa IGP, Ernest Mangu na nakala kutumwa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, kwa waangalizi wa kimataifa na vyombo vya habari.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa NEC kurekebisha tangazo wanalotoa kuhusu matokeo ya kura kwa sababu yamekuwa yakionyesha kumpendelea zaidi mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.

“Naomba tangazo hilo liboreshwe kwa sababu linampendelea Dk. Magufuli kwa kuwa wamekuwa wakiweka zaidi matokeo yanayomuonyesha mgombea wa CCM sehemu ambazo amekuwa akishinda zaidi, lakini maeneo ninayofanya vizuri haitangazi,” alilalama Lowassa.

Alitoa wito kwa NEC kuhakikisha wanaweka matokeo ya wagombea wote bila upendeleo kama wanavyofanya sasa.

Naye Meneja wa Kampeni wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), John Mrema, alisema kukamatwa kwa vijana hao hakumaanishi kwamba Chadema haitapokea matokeo yanayoendelea kwa sababu walijua hilo litatokea.

Kutokana na hali hiyo, alisema walikuwa na vijana wengi waliokuwa wakifanya kazi hiyo kwa ajili ya kupata matokeo sahihi.

“Tumekuwa tukiendelea kupokea matokeo ya kila eneo kadiri yanavyoendelea kutangazwa kwa kutumia vijana wetu wengine waliopo maeneo mbalimbali,” alisema Mrema.

Alionyesha pia kushangazwa na hatua ya polisi kuwakamata vijana wa Chadema na kuwaacha wale wa CCM wanaofanya kazi kama hiyo walioko eneo la Mlimani City.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema ni kweli waliwakamata vijana hao ambao wanawahoji kwa uchunguzi zaidi.

“Tumewakamata watu hao kwa uchunguzi zaidi,  mbaya zaidi watu hao wengine walikuwa si Watanzania, tunawahoji kama wana mawasiliano na NEC na wanalipwa na nani ili kufanya kazi hiyo,” alisema Kova.

Alisema shughuli ya kukusanya matokeo na kuyasambaza kwa raia ni uchochezi kwa kuwa taarifa hizo zinaweza kutumika kuchochea wananchi.

“Walikamatwa kwenye mahoteli tofauti waliyokuwapo na tunawachunguza, na kama hawana makosa tutawaachia na tukiwakuta nayo, sheria itafanya kazi yake.

“Kimsingi hatumwonei mtu, tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Kova.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles