23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

CCM: Tumeshinda majimbo 176

january-makambaVERONICA ROMWALD NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitangazia ushindi wa majimbo 176 kati ya 264 nchini ambayo yamejumlishwa katika matokeo yaliyobandikwa katika vituo mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM Januari Makamba, alisema chama hicho kimefanikiwa kukomboa majimbo 12 yaliyokuwa yakishikiliwa na vyama vya upinzani.

“Kwa kuwa matokeo yamebandikwa hadharani na yamesainiwa na mawakala na wakapewa nakala, CCM hadi sasa tumepata majimbo 176 kati ya 264 na 12 kati ya hayo tuliyoongoza yalikuwa chini ya upinzani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makamba aliwataka wana- CCM kupuuza matokeo yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii, na kwamba matokeo rasmi yatatangzwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Tunawaomba watu wayapuuze matokeo hayo kwa sababu tumebaini bahati mbaya wenzetu wanatoa matokeo ya uongo mapema ili tume ikitoa yaliyo rasmi waseme wameibiwa kura ili kutafuta kisingizio cha kuingia mitaani na kufanya vurugu.

“Pia tumebaini jitihada na nguvu kubwa za wapinzani wetu kupeleka kilio chao kwa waandishi wa habari wa nje ya nchi pamoja na mataifa ya nje kwa ujumla, wameajiri magwiji wa propaganda kutoka nje kwa fedha nyingi ili kujenga taswira kwenye jumuiya ya kimataifa kwamba Tanzania ni kama nchi nyingine barani Afrika ambako hakuna ustaarabu wala utaratibu wa kidemokrasia na Serikali hukandamiza watu wake,” alisema.

Alisema mkakati wa wapinzani ni kuitaka jumuiya ya kimataifa itumie nguvu yake ya misaada kwa Tanzania kulazimisha matokeo ambayo hayatokani na utashi wa wananchi, na kwamba CCM haiko tayari kulikubali jambo hilo.

Akizungumza suala la Zanzibar ambako mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amejitangazia matokeo kuwa ameshinda, alisema CCM wanayapuuza kwani hayajatangazwa na mamlaka husika.

“CCM tunayapuuza na tunaona huu ni mzaha na ndiyo maana tunawasisitiza wananchi wayapuuze kwa sababu anayestahili kutangaza ni Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“Tunahimiza utulivu kwa wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla na waziachie mamlaka husika zifanye kazi yake, hasa katika kipindi hiki kigumu cha kupokea matokeo na kazi ya tume ni kuyatangaza,” alisema.

Alisema mamlaka za mawasiliano zikumbuke wajibu wake katika kusimamia mitandao ya kijamii na kwamba wananchi wafuate kurasa sahihi za vyombo vya habari kupata taarifa sahihi za matokeo.

Makamba alisema changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha uchaguzi kamwe haziwezi kubadili utashi wa wapigakura, na kwamba haziwezi kubeba chama chochote cha siasa.

“Cha msingi wananchi wawe watulivu kwa sababu tunaingia katika kipindi kigumu zaidi cha kupokea matokeo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles